1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
17 Julai 2020

Yaliyozingatiwa kwenye magazeti ya Ujerumani juu ya Afrika wiki hiii ni pamoja na wanajeshi wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani waliokumbwa na maambukizi ya virusi vya corona katika Jamuhuri ya Afrika ya Kati.

https://p.dw.com/p/3fTiz
Friedensnobelpreisträger, UN Blauhelme
Picha: Getty Images/S.Kambou

die tageszeitung

Tunaanza moja kwa moja na gazeti la die tageszeitung juu ya wanajeshi wa Umoja wa Mataifa waliokumbwa na maambukizi ya virusi vya corona katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. Gazeti hilo linasema kati ya askari wapatao 200 miongoni mwa 10,000 wamekumbwa na maambukizi ya corona. Askari mmoja ameshakufa kutokana na maradhi ya COVID -19.

Gazeti la die tageszeitung linasema kuambukizwa kwa wanajeshi hao kunaathiri jukumu lao la kulinda amani katika nchi hiyo ya Afrika ya kati. Gazeti hilo linaarifu kwamba tangu kufumuka kwa janga la corona makundi yenye silaha yamezidi kuteka maeneo nchini humo. Gazeti hilo limemnukulu mkuu wa kikosi cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, Mankeur Ndiaye akieleza kwamba kazi za wanajeshi hao zimesimama kwa muda wa miezi kadhaa kutokana na janga la corona.

Neues Deutschland

Gazeti la Nues Deutschland linatuarifu juu ya maandamano yaliyofanywa mjini Berlin na wakimbizi kutoka Eritrea, kutetea haki ya kuwaleta nchini Ujerumani ndugu na jamaa zao. Gazati hilo linatufahamisha kwamba wakimbizi 1200 kutoka Eritrea wanasubiri ndugu zao waruhusiwe waje Ujerumani ili waungane nao. Gazeti linaeleza kwamba kwa mujibu wa sheria, mkimbizi anayepeta kibali cha kuishi nchini Ujerumani anayo haki ya kuileta familia yake.

Hata hivyo gazeti la Neues Duetschland linatilia maanani kwamba ndugu hao wanakabiliwa na vizingiti virefu kwa sababu hawana hati wanazopaswa kuziwasilisha kwenye balozi za Ujerumani. Jamaa za wakimbizi hao kutoka Eritrea wanasubiri nchini Ethiopia, Kenya na Sudan. Gazeti hilo la Neues Deutschland linatueleza kwamba serikali ya Eritrea ndiyo yenye mamlaka ya kuhalalisha vyeti vya ndoa na vyeti vya kuzaliwa watoto. Hata hivyo gazeti hilo linasema serikali ya Eritrea inatoa hati muhimu kwa wananchi wao wanaoishi nje ya Eritrea kwa masharti kwamba kila mmoja mwenye kipato anapaswa kutoa asilimia 2 ya kipato chake kama kodi kwa serikali ya Eritrea.

Kölner Stadt Anzeiger

Gazeti la Kölner Stadt-Anzeiger linakumbusha kwamba mitaa kadhaa kwenye jiji la Cologne bado inakumbusha enzi ya ukoloni barani Afrika. Linasema baada ya kifo cha George Floyd nchini Marekani mjadala mkali umezuka katika jiji hilo juu ya majina ya mitaa hiyo. Mfano ni mtaa unaoitwa "wa mtu mweusi" katika jiji hilo "the moor street." Gazeti la Kölner Stadt-Anzeiger linatukumbusha kwamba baadhi ya mitaa katika jiji la Cologne ilipewa majina ya wakoloni wa kijerumani, kama Carl Peters na Adolf Lüderitz waliotenda ukatili mkubwa kwa waafrika.

Gazeti la Kölner Stadt- Anzeiger linasema baada ya kifo cha George Floyd nchini Marekani mjadala mkali umezuka juu ya kuyabadilisha majina ya mitaa hiyo. Gazeti hilo linakumbusha kwamba mnamo mwaka 1991 mtaa wa Lüderitz ulibadilishwa na kuitwa Usambara na ule wa Carl Peters ulibadilishwana kuitwa mtaa wa Namibia.

Gazeti linasema mabadiliko yalifanyika kwa makosa lakini nia ilikuwa njema. Kwa sababu Carl Peters hakwenda Namibia na Adolf Lüderitz hakuwapo Tanganyika. Ndiyo kusema kwamba Carl Peters ingekuwa Usambara na Lüderitz ingekuwa Namibia. Gazeti la Kölner Stadt-Anzeiger linatuarifu kwamba baada ya harakati za kupinga kuuliwa kwa mtu mwenye  asili ya Afrika nchini Marekani George Floyd, wahusika mjini Cologne wanatafakari iwapo majina ya mitaa fulani itapaswa ibadilishwe.

Berliner Zeitung

Gazeti la Berliner linasema bara la Afrika halikukumbwa vibaya na maambukizi wa virusi vya corona kulinganisha na Marekani, Ulaya na Amerika ya kusini. Hata hivyo gazeti hilo linasema kiuchumi watu wengi wameathirika, sababu ni kwamba serikali za nchi za Afrika hazina uwezo wa kuwalipa watu wakiwa wamekaa nyumbani bila ya kufanya kazi. 

Vyanzo: Deutsche Zeitungen