1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

5 Juni 2020

Yaliyoandikwa kwenye magazeti ya Ujerumani juu ya masuala na matukio ya barani Afrika ni pamoja na kuathirika kwa uchumi wa Afrika kutokana na janga la corona.

https://p.dw.com/p/3dJSa
Grenze zwischen Lagos und Ogun - Polizeikontrolle
Picha: Getty Images/AFP/P. Utomi Ekpei

HANDELSBLATT:

Gazeti la Handelsblatt linaloelezea wasiwasi juu ya kuathirika kwa uchumi wa nchi za Afrika kutokana na janga la maambukizi ya virusi vya corona. Gazeti hilo linasema mamilioni ya watu watatumbukia katika umasikini zaidi. Gazeti hilo linasema janga la corona limesababisha mgogoro mkubwa wa kiuchumi katika nchi zote duniani lakini nchi za Afrika zimekumbwa zaidi. Gazeti la Handesblatt linaeleza kwamba nchi za Afrika zina uwezo mdogo wa kutenga fedha kwa ajili ya kuzikwamua shughuli za uchumi. Handelsblatt linatilia maanani kwamba hata zile nchi za Afrika zinazouza mafuta kama vile Nigeria kwa sasa zimo katika hali ngumu kutokana na bei ya mafuta kuanguka kwenye soko la dunia. Gazeti hilo linahofia kwamba sekta muhimu za kijamii kama vile za elimu na afya zitarudi nyuma.

DIE ZEIT:

Gazeti la Die Zeit linatupeleka Sudan. Linasema aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo dikteta Omar al Bashir bado anasubiri kuhukumiwa lakini linasema mpaka sasa hakuna uhakika iwapo Bashir atafunguliwa mashtaka juu ya mauaji ya halaiki. Gazeti la Die Zeit linasema watu nchini Sudan wanajiuliza iwapo Omar Bashir ahukumiwe nchini humo au apelekwe kwenye mahakama ya kimataifa ya mjini The Hague? Gazeti hilo linaeleza kwamba kukamatwa kwa Bashir kunaweza kuzingatiwa kuwa ni ushindi kwa wapenda haki lakini linasema mambo siyo rahisi. Hayo wanatambua pia wale waliojitokeza kuandamana na kusababisha kuangushwa kwa utawala wake. Jee Omar Bashir atawajibishwa kwa uhalifu gani? Wanajeshi waliomo kwenye baraza la uongozi, wanalumbana na wawakilishi wa raia juu ya suala hilo. Na jambo la kulitilia maanani, linaeleza gazeti la Die Zeit ni kwamba wanajeshi wamesema hawatampeleka Bashir kwenye mahakama ya kimataifa ya mjini The Hague.

Infografik Coronafälle Afrika 15. Mai 2020 EN
Idadi ya visa vya corona Afrika kufikia Mei 15, 2020.

Gazeti hilo linaeleza kwamba mahakama ya nchini Sudan, imemfungulia mashtaka Omar al Bashir dhidi ya ufisadi na siyo dhidi ya mauaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya binadamu. Dikteta huyo wa zamani anazingatiwa kuwa mutuhumiwa mkuu wa mauaji ya halaiki katika jimbo la Darfur.

DIE TAGESZEITUNG:

Gazeti la die tageszeitung limeandika juu ya Felicien Kabuga, mtuhumiwa wa mauaji ya kimbari ya nchini Rwanda ya mwaka 1994. Kabuga alikamatwa nchini Ufaransa mwezi uliopita baada ya kuukwepa mkono wa sheria kwa muda wa miaka mingi. Gazeti hilo linasema Kabuga anatarajiwa kupelekwa kwenye mahakama maalumu ya Umoja wa Mataifa ya mjini Arusha, inayoshughulikia kesi za mauaji ya kimbari ya nchini Rwanda. Hata hivyo gazeti la die tageszeitung linaarifu kwamba mawakili wa Kabuga wanaweza kuupinga uamuzi huo wa kumpeleka Kabuga kwenye mahakama ya mjini Arusha. Gazeti linaeleza kwamba Kabuga amekana kuhusika na mauaji ya mwaka 1994.

NEUE ZÜRCHER:

Gazeti la Neue Zürcher linasema hadi hivi karibuni mitaa ya mji mkuu wa Senegal, Dakar ilikuwa imejaa watoto ombaomba lakini sasa wamepungua kutokana na hofu ya maambukizi ya virusi vya corona. Gazeti hilo linasema kwa mujibu wa makadirio wako watoto ombaomba 30,000 katika mji wa Dakar. Gazeti la Neue Zürcher linaeleza kwamba watoto hao hutumwa na waalimu wao wa madrasa kuomba fedha barabarani na kuzipeleka kwa waalimu hao. Gazeti hilo linasema hatua za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona zimesaidia juhudi za serikali na mashirika ya misaada za kuwandoa watoto hao barabarani.Gazeti la Neue Zürcher linasema katika mazingira ya kawaida yaani bila ya janga la corona juhudi hizo hutatizwa na itikadi potofu za wazazi wao, lakini gazeti hilo pia limegundua kwamba hao wanaojiita walimu wa madrasa wanaowatuma watoto hao kuombaomba hawana elimu yoyote ya dini.

 

Vyanzo: Deutsche Zeitungen