1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
28 Februari 2020

Yaliyozingatiwa kwenye magazeti ya Ujerumani mnamo wiki hii ni pamoja na habari za kuleta matumaini nchini Sudan Kusini baada ya viongozi wa nchi hiyo kufikia makubaliano ya kuunda serikali ya kugawana mamlaka.

https://p.dw.com/p/3Ybiu
Südsudan Salva Kiir und Riek Machar | Entscheidigung für  Einheitsregierung
Picha: AFP/A. McBride

die tageszeitung

Rais Salvar Kirr na hasimu wake mkubwa Riek Machar wamekubaliana kushirikiana katika kuongoza serikali mpya ya Sudan Kusini, ambapo Machar atakuwa makamu wa rais. Hata hivyo mchakato huo wa kugawana mamlaka hautakuwa rahisi. Serikali hiyo mpya ya umoja wa kitaifa itasimamia kipindi cha mpito cha miaka mitatu hadi hapo uchaguzi utakapofanyika.

Hata hivyo gazeti la die tageszeitung linakumbusha kwamba bado yapo matatizo kadhaa yanayopaswa kutatuliwa ili kuweza kufanikisha utekelezaji wa makubaliano hayo mapya. Kwanza ni suala la kugawana mamlaka baina ya rais Salva Kiir na hasimu wake Riek Machar  wanaotoka makabila tofauti. Na pili ni jinsi ya kuwaunganisha wapiganaji wao jumla ya 38,000 na kuwa jeshi  la taifa.

Die Welt

Gazeti la Die Welt linamzungumzia hayati Hosni Mubarak. Rais wa zamani wa Misri aliyefariki wiki iliyopita akiwa na umri wa miaka 91. Gazeti  hilo linasema licha ya kuondolewa madarakani kutokana na harakati za wananchi, Mubarak aliaga dunia akiwa mtu huru kabisa. Gazeti hilo linaeleza kwamba alipokuwa madarakani kuanzia mwaka 1981 hadi 2011 Mubarak alifanikiwa kuzibadilisha itikadi za hapo awali na kuzitumia kwa ufanisi na hivyo kuweza kukubalika kama mshirika muhimu wa Marekani na nchi za magharibi kwa jumla.

Mubarak alidumisha amani na Israel na hivyo kueonekana kuwa kiongozi aliyehitajika sana na nchi za magharibi. Baada ya rais wa Misri wa hapo awali Anwar Sadat kuuliwa na mtu aliyehusiana na magaidi walioufuata uislamu wa itikadi kali, Mubarak alijenga mfumo wa usalama kwa lengo la kuwadhibiti wafuasi wa itikadi kali za kidini.

Gazeti hilo linakumbusha kwamba Sadat aliuliwa na magaidi ambao hawakutaka Misri itie saini mkataba wa amani na Israel na linasema baada ya kuingia madarakani mnamo mwaka 1981 Mubarak alitambulika kwa sera yake kali ya kuwaandama watu waliokuwa wanafuata uislamu wa itikadi kali. Sera hiyo bado inatekelezwa hadi leo na rais Abdelfattah al-Sisi. Iwapo ni sawa kwa al Sisi kuifuata sera hiyo, ni  swali ambalo wahusika katika nchi za magharibi wanapaswa kujiuliza wanapozungumia juu ya siasa za mashariki ya kati.

Süddeutsche 

Nalo gazeti la Süddeutsche linatahadharisha juu ya hatari inayosababishwa na nzige katika nchi za Afrika Mashariki. Gazeti hilo linasema uvamizi wa wadudu hao unaweza kuleta madhara makubwa. Pana hatari kubwa ya wakulima kukosa mavuno. Na jambo linalosababisha wasiwasi mkubwa ni kwamba serikali za nchi za Afrika Mashariki hazina uwezo mkubwa wa kukabiliana na baa la wadudu hao waharibifu.

Gazeti la Süddeutsche limelinukulu shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO likitahadharisha kwamba katika miezi ijayo sehemu nyingi za Afrika Mashariki zitakabiliwa na uhaba wa chakula kutokana na ukosefu wa mavuno. Thuluthi mbili ya watu katika Afrika Mashariki wanategemea kilimo ili kukimu maisha yao.

Weser Kurier

Gazeti la Weser Kurier limesisitiza juu ya kuchukuliwa hatua kali dhidi ya nchi nchi zinazopeleka silaha na wapiganaji katika nchi ya Libya licha ya kuwepo marufuku ya Umoja wa Mataifa. Gazeti hilo linaeleza kwamba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa baada ya kikao chake cha siku ya Jumatano limetoa kauli kwamba hakuna mtu au nchi itakayovumiliwa kwa kukiuka vikwazo vya silaha dhidi ya Libya.  Gazeti hilo la Weser Kurier linasema mpango wa Umoja wa Ulaya wa kuzuia silaha kuingia nchini Libya unapaswa kuhakikisha kuwa shinikizo kwa wauzaji wa silaha linaongezeka. 

Vyanzo: Deutsche Zeitungen