1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
21 Februari 2020

Masuala na matukio ya barani Afrika yaliyozingatiwa kwenye magazeti ya Ujerumani mnamo wiki hii ni pamoja na ziara ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo katika nchi tatu za Afrika. 

https://p.dw.com/p/3Y7MY
Mike Pompeo  in Äthiopien
Picha: Getty Images/A. Caballero-Reynolds

Neue Zürcher

Gazeti la Neue Zürcher linasema waziri Pompeo alipaswa kujionea mwenyewe jinsi China ilivyojitanua barani Afrika.Katika ziara hiyo Pompeo alikwenda Senegal, Angola na Ethiopia. Aliweza kujionea kwa macho yake kwamba China ndiyo mshirika mkubwa wa biashara wa nchi za Afrika na siyo tena Marekani au washirika wake wa Ulaya magharibi. Mgeni huyo kutoka Marekani aliona miundombinu kama njia za reli na barabara zilizojengwa kutokana na mikopo kutoka China. Gazeti la Neue Zürcher linasema licha ya kutoa kauli tupu waziri Pompeo hakuwa na lingine la kuipa Afrika na ndiyo kwanza Marekani imetangaza kuyaondoa majeshi yake yaliyokuwa yanasaidia katika harakati za kupambana na magaidi Afrika magharibi.

Süddeutsche

Gazeti la Süddeutsche linasema Ujerumani haina meli za kutosha kwa ajili ya kushiriki katika juhudi za Umoja wa Ulaya za kuzuia silaha kuingia nchini Libya. Gazeti hilo linaeleza kwamba Ujerumani haina meli za kutosha ili kuweza kushiriki katika ulinzi wa pwani ya Libya katika juhudi za Jumuiya hiyo za kulitekeleza azimio la Umoja wa Mataifa la kuiwekea Libya vikwazo vya silaha. Kwa mujibu wa wataalamu haitawezekana kwa Ujerumani kutoa mchango wake katika zoezi hilo baada ya nchi za Umoja wa Ulaya kukubaliana kupeleka meli kwenye pwani ya Libya. Kati ya manowari tisa zilizopo kwa sasa ni tatu tu zinazoweza kutumika bila ya matatizo. Ujerumani ilifurahia habari kwamba Umoja wa Ulaya umekubali kubeba jukumu kubwa zaidi katika juhudi za kuleta amani nchini Libya.

Gazeti la Süddeutsche limemnukulu Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas akisema, pamoja na ulinzi wa kutokea angani, meli pia zinapaswa kutumika katika harakati za kuzuia silaha kuingia Libya. Hata hivyo gazeti hilo linasema kwa sasa Ujerumani haiwezi kubeba majukumu mengine. 

Derr Tagesspiegel

Nalo gazeti la Der Tagesspiegel linatupeleka Afrika Kusini ambako rais wa zamani wa utawala wa  wazungu FW de Klerk ametifua tufani! linaeleza kwamba Rais huyo wa zamani de Klerk alisema kwenye mahojiano ya televisheni kwamba mfumo wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini haukuwa wa uhalifu dhidi ya ubinadamu. Kauli ya bwana de Klerk imewakasirisha watu wengi miongoni mwao, wabunge wa chama kinachotetea ukombozi wa kiuchumicha, EFF. Wabunge wa chama hicho wanataka bwama de Klerk avuliwe nishani ya amani ya Nobel  aliyotunukiwa pamoja na Nelson Mandela. Mnamo mwaka 1993 tayari mjadala mkali ulizuka nchini Afrika Kusini ambapo watu walilalamika ni kwa nini de Klerk alitunukiwa nishani hiyo pamoja na kiongozi wa harakati za ukombozi Nelson Mandela. Gazeti la Der Tagesspiegel linakumbusha kwamba utawala wa de Klerk ulihusika na mauaji ya maalfu ya watu weusi.

Frankfurter Allgemeine

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linatuarifu juu ya juhudi za kupambana na nzige katika nchi za Afrika mashariki linasema Umoja wa Mataifa umeahidi kutoa dola milioni 76 kwa ajili ya harakati za kupambana na nzige, hata  hivyo mpaka sasa ni dola milioni 20 zilizopatikana. Umoja wa Ulaya pia umetoa dola milioni moja na  Marekani dola laki nane! Umoja wa Mataifa umetahadharisha kwamba watu milioni 13 wamo katika hatari ya kukumbwa na njaa kutokana na mashamba kuvamiwa na nzige. Kenya inatumia ndege kupambana na  wadudu hao na nchini Uganda waziri wa kilimo amesema wanajeshi wanapatiwa mafunzo maalumu ili kuweza kuwakabili wadudu hao.

Vyanzo: Deutsche Zeitungen