1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
7 Februari 2020

Masuala na matukio ya barani Afrika yaliyozingatiwa na magezti ya Ujerumani mnamo wiki hii ni pamoja na ziara ya kansela wa Ujerumani Angela Merkel katika nchi za Afrika Kusini na Angola.

https://p.dw.com/p/3XPzo
Südafrika Angela Merkel und Cyril Ramaphosa
Picha: Reuters/S. Sibeko

Bild

Gazeti la Bild limeandika juu ya ziara ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel nchini Afrika Kusini na Angola. Gazeti hilo linakumbusha kwamba hii ni mara ya tatu Kansela Merkel amefanya ziara nchini Afrika Kusini. Hata hivyo gazeti hilo linasema bibi Merkel amefanya ziara wakati ambapo mwenyeji wake rais Cyril Ramaphosa ametingwa na matatizo ndani ya chama chake.

Gazeti hilo linaeleza kwamba uchumi wa Afrika kusini umedhoofika wakati ambapo rais Ramaphosa anapaswa kushughulikia mivutano ya ndani ya chama chake tawala, African National Congress, ANC. Uchumi wa Afrika Kusini haujaonyesha dalili za kustawi wakati asilimia 60 ya vijana wa nchi hiyo hawana ajira. Hata hivyo inapasa  kutilia maanani kwamba biashara kati ya Afrika Kusini na Ujerumani inafikia thamani ya Euro Bilioni 17.

Gazeti la Bild linatufahamisha kwamba Kampuni zipatazo 600 za Ujerumani zinafanya biashara katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika. Ujerumani inashika nafasi ya pili katika kufanya biashara na Afrika Kusini baada ya China na Marekani. Gazeti hilo limetilia maanani kwamba katika ziara yake safari hii Kansela  Merkel alijadili zaidi masuala ya kiuchumi na wenyeji wake wa Afrika Kusini na Angola badala ya suala la uhamiaji. 

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung ambalo linatupasha habari juu ya uamuzi wa mahakama kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa rais uliofanyika mwaka jana nchini Malawi nalinasema uamuzi wa mahakama ya katiba nchini Malawi kubatilisha ushindi wa rais Peter Mutharika ni ushindi wa demokrasia. Uamuzi huo nchini Malawi unaweka kigezo kipya katika chaguzi za barani Afrika, baada ya uamuzi kama huo kupitishwa nchini Kenya mnamo mwaka 2017. Mahakimu nchini Malawi wameeleza kwamba waliufikia uamuzi huo baada ya kubainika kwamba udanganyifu ulifanyika wakati wa kuhesabu kura mwaka uliopita.

Die Welt

Gazeti la Die Welt linasema walioahidi kuacha kupeleka silaha nchini Libya hawakusema kweli. Ahadi hiyo ilitolewa kwenye mkutano uliofanyika mjini Berlin hivi karibuni kuujadili mgogoro wa nchini Libya. Gazeti la Die Welt linaeleza kwamba kila siku ndege za mizigo zinatua nchini Libya. Kwa upande mmoja ni ndege zinazotua katika sehemu ya Libya inayodhibitiwa na jenerali Khalifa Haftar. Na katika upande mwingine ni ndege zinazopeleka zana za kivita kwa ajili ya serikali ya Libya inayotambuliwa na jumuiya ya kimataifa.

Vikwazo vya silaha vilivyowekwa na Umoja wa Mataifa vinaendelea kukiukwa. Inapasa kukumbuka kwamba siku chache tu zilizopita wajumbe wa pande zinazohusika na mgogoro wa nchini Libya walikutana mjini Berlin na kuahidi kuacha kupeleka silaha nchini humo.

Gazeti la Die Welt linasema mataifa ya nje yanaendelea kupeleka silaha na wapiganaji nchini Libya. Linaeleza kuwa makubaliano yaliyofikiwa kwenye mkutano wa Berlin yamo hatarini kusambaratika, kwa sababu hakuna anayethubutu kuzitaja hadharani nchi zinazokiuka vikwazo vya silaha dhidi ya Libya vilivyowekwa na Umoja wa Mataifa tangu mwaka 2011.

Badische

Kuna habari za kufurahisha zilizoandikwa na gazeti la Badische kuhusu mafanikio yaliyopatikana katika kupambana na ujangili nchini Afrika Kusini. Gazeti hilo limeandika kwamba idadi ya Faru waliouliwa na majangili mwaka uliopita ilizidi kupungua nchini Afrika Kusini. Mnamo mwaka 2018 wanyama pori hao 769 waliuliwa na majangili kwa sababu ya pembe zao. Lakini mwaka jana idadi ilipungua hadi 594. Waziri wa ulinzi wa mazingira wa Afrika Kusini amesema ujangili umepungua katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kutokana na kazi nzuri ya walinzi wa wanyama pori.

Hata hivyo gazeti la Badische linasema mafanikio makubwa zaidi yatapatikana katika harakati za kupambana na ujangili nchini Afrika Kusini iwapo nchi zote duniani zitashirikiana. Kwa mujibu wa taarifa barani Afrika kote wamebakia faru 7000 tu. Biashara kubwa ya pembe za wanyamapori inafanyika katika nchi za Asia na hasa China na Vietnam.

Vyanzo: Deutsche Zeitungen