1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Gakuba, Daniel   
17 Januari 2020

Yaliyoandikwa kwenye magazeti ya Ujerumani kuhusu Afrika ni pamoja na juhudi zinazofanywa na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron katika kuziimarisha nchi za ukanda wa Sahel kukabiliana na baa la ugaidi kwa ufanisi.

https://p.dw.com/p/3WLSO
Frankreich l Macron wirbt für Sahel-Initiative
Picha: Reuters/G. Horcajuelo

Süddeutsche

Rais Macron alikutana na viongozi wa Mauritania, Mali, Burkina Faso, Niger na Chad hata hivyo gazeti la Süddeutsche linasema juhudi kubwa zaidi zitahitajika na linaeleza kwamba mkutano huo wa rais Macron na viongozi kutoka nchi tano za ukanda wa Sahel umeonyesha wazi kwamba harakati za kupambana na ugaidi kwenye ukanda huo siyo tena tatizo la nchi hizo za Afrika pekee.

Ndiyo Sababu mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Josep Borrel na rais wa baraza la Umoja huo Charles Michel pia walishiriki. Gazeti la Süddeutsche linafahamisha kwamba viongozi wa nchi za Sahel pia wamealikwa kushiriki kwenye mkutano wa kilele wa nchi za Umoja wa Ulaya mwishoni mwa mwezi Machi utakaofanyika mjini Brussels.

Mapambano dhidi ya magaidi kwenye ukanda wa Sahel itakuwa mojawapo katika ajenda ya Umoja wa Ulaya na kila nchi mwanachama itapaswa kueleza ni mchango gani itakaotoa. Gazeti la Süddeutsche limekumbusha hatari ya magaidi iliyoonekana tena wiki iliyopita kutokana na kuuliwa wanajeshi 90 wa Niger.

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung linatupeleka Sudan ambako maafisa wa zamani wa kikosi maalumu walifanya uasi. Uasi wa maafisa hao waliokuwa watiifu kwa aliyekuwa rais wa Sudan Omar Bashir unathibitisha kwamba hata baada ya nguvu ya utawala wa kijeshi kupungua, Sudan bado ina safari ndefu hadi kufika kwenye utulivu wa kweli. Jeshi liliuzima uasi huo. Maafisa hao walipaswa kuondoka kwenye kambi mbili za kijeshi kwa sababu kikosi chao kilikuwa kinavunjwa. Waliambiwa wachague ama kujiondoa kwenye kikosi hicho au kujiunga na kikosi kingine cha dharura. Lakini waliyakataa yote hayo.

Gazeti la die tageszeitung linatueleza kuwa waasi hao walikataa fidia iliyokuwa walipwe na pia walitaka kuendelea kuwamo katika jeshi la Sudan. Lakini kutokana na mageuzi yanayofanywa ndani ya jeshi hilo idara ya maafisa hao nayo imefanyiwa mabadiliko na juu ya mageuzi hayo gazeti la die tageszeitung linaeleza kwamba Waziri Mkuu Abdallah Hamdok ni kiongozi aliyesimama mstari wa mbele katika kuleta mageuzi kwenye jeshi la Sudan. Sababu ni kwamba maafisa waliofanya uasi wametoka kwenye idara iliyokuwa sehemu ya chombo cha ukandamizaji kilichotumiwa na Omar Bashir.

Die Welt

Gazeti la Die Welt wiki hii linafichua ukweli juu za suala la wakimbizi kutoka Afrika na kwa ajili hiyo gazeti hilo limefanya mahojiano na mkuu wa kitengo cha shirika la uhamiaji duniani IOU, nchini Ethiopia. Mkuu huyo Maureen Achieng ameliambia gazeti hilo kwamba watu barani Ulaya wanazidi kuwa na hofu juu ya wakimbizi wanaoweza kukimbilia katika bara lao. Hali hiyo inasababisha hofu hasa juu ya wakimbizi kutoka Afrika.

Katika mahojiano hayo mwakilishi huyo wa shirika la uhamiaji duniani nchini Ethiopia bibi Achieng ameliambia gazeti la Die Welt kuwa picha inayotolewa juu ya wakimbizi wa Afrika siyo kamili. Gazeti la Die Welt limemnukulu mwakilishi huyo akieleza kuwa zaidi  ya asilimia 85 ya wakimbizi wa Afrika ni wale wanaokwenda katika nchi nyingine za Afrika. Bi Maureen Achieng amesema serikali za Afrika na Ulaya zinapaswa kuzungumza vizuri na wananchi wao juu ya suala la wakimbizi.

die tageszeitung

Mwaka huu unatimia wa 50 tangu vita vya Biafra vimalizike nchini Nigeria. Jee vita hivyo vilisababishwa na kitu gani? Gazeti la die tageszeitung linatueleza kwamba watu wa jimbo la Biafra la kusini mashariki mwa Nigeria mnamo mwaka 1967 walianzisha harakati za kupigania kujitenga na serikali kuu ya Nigeria baada ya watu wa sehemu hiyo wa kabila la Waigbo kuhisi kuwa walikuwa wanabaguliwa. Walihisi kuwa watu wa jimbo lao hawakuweza kuwa sehemu ya Nigeria kwa sababu serikali kuu ilikuwa inadhibitiwa na viongozi kutoka kaskazini.

Gazeti hilo linatilia maanani kwamba vita hivyo siyo tena suala linalozungumziwa nchini Nigeria ingawa vilisababisha vifo vya watu kati ya laki tano na milioni tatu linasema katika mwaka wa 50 tangu kumalizika vita hivyo vya Biafra hakuna shughuli zozote rasmi zinazofanywa kukumbusha juu ya maafa yaliyosababishwa na vita hivyo.

Vanzo:/Deutsche Zeitungen