Afrika katika magazeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 27.09.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Ujerumani

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Wiki hii yaliyoandikwa kwenye magazeti ya Ujerumani juu ya Afrika ni pamoja na mahojiano na mtaalamu wa masuala ya Misri kuhusu maandamano yaliyofanyika nchini humo ya kumtaka al Sisi aachie madaraka.

Der Tagespiegel

Gazeti la Der Tagesspiegel linasema watu wanaofanya maandamano ya kumpinga Rais wa Misri Abdel Fatah al-Sisi wanajua vyema kile kinachoweza kuwafika. Wanaweza kukamatwa, kufungwa na hata kukabiliwa na hatari ya kupigwa risasi. Sababu ya watu  hao kujitokeza barabarani ni kuongezeka kwa umasikini. Thuluthi moja ya watu nchini Misri wanaishi katika hali duni. Licha ya serikali kujaribu kupuuza maandamano hayo, itapaswa kutoa jibu.

Mtaalamu huyo ameliambia gazeti la Der Tagesspiegel kwamba waandamanaji wamejitayarisha vizuri na wanazungumzia juu ya mapinduzi mengine baada ya kuondolewa madarakani kwa Rais wa hapo awali Hosni Mubarak. Wamisri wanasema Rais al-Sisi anatawala kwa njia ya kuwaweka rafiki zake kwenye nafasi  muhimu za  jeshi.

Süddeutsche

Nalo gazeti la Süddeutsche wiki hii limeandika juu ya harakati za mwanamuziki maarufu nchini Uganda Bobi Wine. Gazeti hilo linasema Bobi Wine sasa anaimba nyimbo za kumkosoa Rais Yoweri  Museveni na utawala wake na linaeleza kwamba mambo sasa yamebadilika kwa mwanamuzuki huyo. Hapo awali Bobi Wine alikuwa anaimba nyimbo  juu ya mapenzi. Lakini sasa nyimbo zake zina maudhui ya kisiasa. Sasa anawania kuwa Rais wa Uganda ili kuundoa utawala wa Museveni kwa ajili ya kuuondoa ufisadi na viongozi waliojibandika madarakani.

Gazeti la Süddeutsche limemnukulu Bobi Wine akisema bila ya msaada kutoka nchi za magharibi utawala wa Museveni usingeliweza kusimama. Watu wa Uganda wamesubiri kwa muda mrefu na sasa umefika wakati wa vijana nchini Uganda kwani vijana ndio viongozi wa kesho. Msemo kwamba macho ya mzee yanaona vizuri zaidi hauna mashiko tena. Vijana wanastahili kusikilizwa. Museveni aliyekaa madarakani kwa miaka 33 anahofia mabadiliko.

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung limeandika juu ya askari watoto nchini Sudan Kusini. Gazeti limebainisha kwamba watoto hao ni wengi kuliko inavyojulikana na linasema kwamba mchakato wa kuleta amani ndio unaosababisha watoto wengi kuandikishwa kama askari Sudan Kusini. Gazeti hilo linaeleza kwamba uchunguzi uliofanywa na tume ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa umebainisha kwamba makundi ya waasi na serikali kadhalika inawaandikisha watoto kama askari. Ni kama jambo la dhihaka kwamba mapatano ya amani yameharakisha uandikishaji wa watoto kama askari.

Rais Salva Kiir na hasimu wake mkubwa Riek Machar wanatarajiwa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa mnamo mwezi Novemba. Mahasimu hao walitia saini mkataba wa amani mwaka uliopita ulioweka msingi wa kuunda serikali hiyo. Gazeti la die tageszeitung linatilia maanani kwamba idadi kubwa ya vijana wanaandikishwa kwenye sehemu ambako mapigano yanazuka mara kwa mara.  Hata hivyo gazeti hilo linasema yapo matumaini tangu kuanzishwa mchakato wa amani. Wakulima wengi wamerejea mashambani katika sehemu kadhaa za Sudan Kusini.

Frankfurter Allagemeine

Gazeti la Frankfurter Allgemeine wiki hii limeandkika juu ya Grace Mugabe, mjane wa aliyekuwa Rais wa Zimbabwe hayati  Robert Mugabe. Gazeti linatuarifu kwamba mama huyo atarithi utajiri uliolimbikizwa na mumewe na linasema ni mtu mmoja tu aliyejitokeza kuwa mshindi baada ya kifo cha Robert Mugabe. Serikali ya Zimbabwe imempa Grace Mugabe haki ya kurithi utajiri wote ulioachwa na Robert Mugabe baada ya kuulimbikiza kwa muda wa miaka 28 alipokuwa madarakani.

Pamoja na vitu vingine vya thamani Grace Mugabe atarithi nyumba inayokadiriwa kuwa ya thamani ya Euro milioni tano. Familia ya Mugabe pia ina mali nchi za nje zenye thamani ya dola Bilioni moja.

Katika upande mwingine gazeti la Frankfurter Allgemeine linatufahamisha kwamba kipato cha wastani nchini Zimbabwe ni dola 130 na ukosefu wa ajira unafikia asilimia 80. Gazeti hilo limemnukulu mtaalamu wa mambo ya uchumi wa Marekani Steve Hanke akisema kwamba kiwango cha mfumuko wa bei kimepanda hadi asilimia 851. 

die tageszeitung

Makala nyingine ya gazeti la die tagszeitung inaangazia juu ya mvutano kati ya  Afrika Kusini na Nigeria. Gazeti hilo limeandika kwamba dunia yote inaangazia macho nchini Afrika Kusini kutokana na kuongezeka kwa mvutano baina ya nchi hiyo na Nigeria. Nchi hiyo ya Afrika magharibi ina mpango wa kuipeleka Afrika Kusini mbele ya Umoja wa Mataifa kutokana na kushambuliwa kwa raia wake waliokuwa wanaishi nchini Afrika Kusini.

Mwenyekiti wa zamu kwenye baraza kuu la Umoja wa Mataifa ni balozi wa Nigeria. Mpaka sasa Nigeria imeshawarudisha nyumbani raia wake 600 kutoka Afrika Kusini waliokuwamo katika hatari ya kushambuliwa. Watu wasiopungua 12 kutoka nchi nyingine za Afrika waliuliwa wiki chache zilizopita baada ya kushambuliwa na wenyeji wanaochukia wageni.

Vyanzo: Deutsche Zeitungen