1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
9 Agosti 2019

Matukio ya barani Afrika yaliyozingatiwa na magazeti ya Ujerumani mnamo wiki hii ni pamoja na habari za kutia moyo kutoka Msumbiji ambako serikali ya nchi hiyo na wapinzani wa Renamo wametia saini mkataba wa Amani.

https://p.dw.com/p/3Nd6u
Mosambik Maputo | Filipe Nyusi und Ossufo Momade unterschreiben Friedensabkommen
Picha: Getty Images/AFP/Stringer

die tageszeitung 

Hatua ya serikali ya Msumbiji na wapinzani wa Renamo ya kutia saini mkataba wa Amani ni  mafanikio siyo tu kwa Msumbiji bali ni kwa bara lote la Afrika linalotafuta masulihisho ya kiafrika kwa matatizo ya barani humo. Mkataba huo unafungua njia ya kuleta Amani baada ya mapambano ya miaka mingi kati ya serikali ya Msumbiji na wapinzani wa Renamo ambao mnamo miaka iliyopita walikuwa  wanaungwa mkono na utawala wa makaburu. Gazeti hilo linasema kutokana na mkataba huo wa Amani Msumbiji sasa itaweza kuzitumia vizuri raslimali zake kwa ajili ya kuleta maendeleo ya kiuchumi.

Gazeti la die tageszeitung limemnukuklu Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi akisema mchakato huo wa Amani hautarudi nyuma wakati kiongozi wa Renamo Ossufo Momade amekaririwa akisema enzi mpya imeanza nchini Msumbiji baada ya mkataba wa Amani kutiwa saini. 

Die Welt

Gazeti la Die Welt wiki hii linauzungumzia mkasa wa Clemens Tönnies mwenyekiti wa baraza la uongozi katika klabu ya kandanda ya ligi kuu ya Ujerumani Schalke na linaeleza kwamba mwenyekiti huyo aliteleza ulimi aliposema "Waafrika waache kuzaana mara giza linapoingia na pia waache kukata  miti". Alisema hayo wakati alipokuwa anakosoa wazo la kupandisha kodi ili kuunga mkono harakati za kupambana na mabadiliko ya tabia nchi. Bwana Tönnies alitamka hayo kwenye hafla rasmi kama kiongozi wa timu maarufu ya kandanda nchini Ujerumani.

Gazeti la Die Welt linatilia maanani kwamba  licha ya kauli hiyo ya kibaguzi baraza la heshima la timu yake ya Schalke O4 limeamua kumpiga teke la kuku tu. Kiongozi huyo wa klabu ya Schalke ameomba radhi na atakaa pembeni kwa muda wa miezi mitatu kabla ya kurudi kwenye kiti chake na kuendelea na kazi yake.

Süddeutsche Zeitung

Gazeti la Süddeutsche wiki hii linatupeleka katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambako linasema madaktari pia wanalazimika kubeba silaha. Gazeti hilo linaeleza kuwa licha ya kuwekwa vituo vipya vya tiba, maambukizi ya virusi vya Ebola bado yanaendelea kuenea nchini humo. Watu wana mashaka juu ya serikali na pia juu ya wasaidizi kutoka nje. Katika sehemu ya mashariki ya Kongo, kwa muda wa miaka mingi watu wameyaona mengi mabaya. Na kuanzia mwaka 1998  makundi mbalimbali yamekuwa yanapigana katika sehemu hiyo ya mashariki. Gazeti la Süddeutsche linakumbusha kwamba tangu kubainika kwa virusi vya Ebola mnamo mwaka 1976 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, milipuko ya maambukizi ilitokea mara 10 lakini wakati wote hali ilidhibitiwa.

Frankfurter Allgemeine

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema Rais wa Rwanda Paul Kagame anajifanya kuwa mtu mwadilifu lakini anawaandama  wapinzani  wake kwa kuwatia ndani na  hata  kuwamaliza:Gazeti hilo limeandika makala juu ya kiongozi  wa upinzani Victoire  Ingabire aliyetaka kuwania kiti cha Rais mnamo mwaka 2010.Gazeti la Frankfurtee Allgemeine  linasema baada ya kuishi nje kwa muda wa miaka 16 Ingabire alirejea Rwanda mnamo mwaka 2010 na alitaka kuwania urais lakini kwanza hakuruhusiwa kushiriki katika uchaguzi.

Baada ya muda mfupi aliwekwa kwenye kuzuizi cha nyumbani na kufikishwa mahakamani siku chache baadae. Hakimu alimtia Ingabire hatiani  kwa kukana mauaji ya kimbari na kwa kula njama za kutaka kuiangusha serikali. Alifungwa kwenye jela ya Mageragere hadi mwezi Septemba mwaka uliopita. Wiki tatu baada ya Ingabire kuachiwa, makamu mwenyekiti wa chama chake Boniface Twagirimana alipotea na Katibu wa Ingabire Anselme Mutuyimana alikutwa ameuawa msituni.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine limemnukulu Victoire ingabire akisema kwamba Kagame anataka kuonekana kuwa mwadilifu. Anataka kuwa kiongozi maarufu barani Afrika na kwa sababu anataka michezo  ya nchi za jumuiya ya madola ifanyike Rwanda, anajaribu kuujenga wajihi wake lakini pembe za chaki wapinzani wanaandamwa na hata kuuliwa. 

Vyanzo/Deutsche Zeitungen/Magazeti ya Ujerumani