1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
3 Mei 2019

Yaliyoandikwa na magazeti ya Ujerumani juu ya masuala na matukio ya barani Afrikani pamoja na ziara ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel katika nchi tatu za eneo la Sahel. Pia yameandika juu ya mgogoro wa nchini Sudan.

https://p.dw.com/p/3Hrl5
Niger Kanzlerin Merkel auf Afrikareise | Merkel und Präsident Issoufou
Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Frankfurter Allgemeine 

Eneo la Sahel, magharibi mwa Afrika limekuwa suala muhimu katika sera ya nje ya Ujerumani. Ni manufaa makubwa kwa Ujerumani ikiwa eneo hilo litakuwa na utulivu kama alivyoeleza msemaji wa serikali ya Ujerumani. Na kila itakapowezekena Ujerumani itazisaidia nchi za sehemu hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Katika ziara yake ya mwaka 2016 Kansela Angela Merkel alizitembelea Niger na Mali lakini safari hii ameziongeza Burkina Faso na Chad katika ratiba ya ziara yake ya barani Afrika. Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema Kansela Merkel anaweka mkazo mkubwa juu ya nchi hizo katika sera yake ya nje hasa kutokana na tatizo la wakimbizi. Gazeti hilo linasema idadi ya wakimbizi wanaokwenda Ulaya kutoka nchi hizo ni ndogo lakini, zinatumika kama njia ya kuanzia safari ya Ulaya na hasa Niger. Gazeti hilo linaeleza kwamba wanajeshi wa Ujerumani pia wanalinda amani nchini Mali kama sehemu ya jeshi la Umoja wa Mataifa.

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung wiki hii limeandika juu ya mgogoro wa  Sudan. Linauliza jee wapinzani watafanikiwa au jeshi litaendelea kushika hatamu. Waandamanaji na wanajeshi nchini Sudan kimsingi wamekubaliana kuunda baraza la pamoja la kusimamia kipindi cha mpito katika nchi hiyo lakini suala la utatanishi linahusu idadi ya wajumbe kutoka kila upande. Harakati za wapinzani bado zinaendelea kwa sababu ufumbuzi bado haujapatikana.

Suala hilo ni muhimu kwa sababu baraza hilo ndilo litakalokuwa na mamlaka makubwa ya kuunda serikali lakini pana mkwamo unaotokana na msimamo wa wanajeshi wa kutaka kuwa na idadi kubwa ya wajumbe kuliko ya raia. Wakati wapinzani wanataka kuwakilishwa na wajumbe angalau wanane katika baraza hilo wanajeshi wanataka kuwapa wapinzani hao nafasi tatu tu.

Hata hivyo gazeti la die tageszeitung limemnukulu makamu mwenyekiti wa chama cha upinzani cha Ummat Mariam al Saddiq akisema njia ya kuelekea kwenye Sudan mpya bado ni ndefu sana na ndiyo sababu Mariam, ambae ni binti yake Waziri Mkuu wa  miaka iliyopita Saddiq al Mahdi amesema wanajeshi bado wanahitajika.

Neue Zürcher

Gazeti la Neue Zürcher linazungumzia juu ya hukumu iliyotolewa na mahakama kuu ya michezo dhidi ya rufaa iliyowasilishwa na mwanamichezo mwanamke wa Afrika Kusini Caster Semenya. Semenya anazingatiwa kuwa mtu mwenye mchanganyiko wa jinsia lakini hilo halijathibitishwa rasmi. Yeye mwenyewe ni msichana na anahisi kuwa mwanamke lakini anacho kiwango cha juu sana cha homoni  za kiume. Wanariadha wengine wamelalamika kuwa Semenya anashinda wakati wote kwa sababu anazo homoni za kiume.

Mahakama ya kimataifa ya michezo imetoa hukumu inayosema ikiwa Semenya anataka kuendelea kushiriki katika mashindano ya michezo atapaswa apunguze kiwango cha homoni. Gazeti la Neue Zürcher linasema hukumu dhidi mwanamke huyo bingwa wa Olimpiki na wa dunia, ina mashaka mengi.

die tageszeitung

Makala nyingine ya gazeti la die tageszeitung inahusu mgogoro wa Libya. Katika safu yake ya maoni gazeti hilo linasema mafuta ya Libya lazima yasusiwe sasa hivi!. Mabomu yanaanguka katika mji mkuu Tripoli. Kwa nini hakuna yeyote anayechukua hatua wakati Libya inabomoka? Sasa umefika wakati wa kuweka vikwazo dhidi ya mafuta ya Libya.

Hatua iliyochukuliwa na Marekani ya kuiwekea vikwazo Iran pia inaweza kuchukuliwa dhidi ya Libya. Ikiwa mafuta ya Libya yatasusiwa wababe wa kivita wa nchi hiyo ndio watakaokomeshwa kwa sababu wao ndiyo wanaotumia fedha za mafuta kununulia silaha.

Vyanzo:/Deutsche Zeitungen