Afrika katika magazeti ya Ujerumani
11 Mei 2018Frankfurter Allgemeine
Mjasiramali kutoka Ufaransa Gregoire Schwebig mwenye umri wa miaka 32 amesema hakuweza kuuona mchakato wa ustawi wa uchumi barani Asia, kwa sababu bado alikuwa mtoto wakati huo. Lakini sasa anataka kushuhudia kwa macho yake ustawi wa uchumi barani Afrika na ndiyo sababu yeye na mkewe waliamua kufungua biashara nchini Kenya na wako huko tangu mwaka wa 2011. Kwa mujibu wa gazeti hilo la Frankfurter Allgemeine, Mfaransa huyo, anafanya kazi ya kusanifu majengo, kuzitafutia kampuni ofisi na kuratibisha shughuli za wafanyabiashara na mahoteli. Schwebig aliliambia gazeti hilo kwamba anaamini bara la Afrika litashuhudia ustawi mkubwa lakini gazeti hilo pia linatilia maanani.
Katika kipindi cha miaka 5 iliyopita idadi ya kampuni za Ufaransa nchini Kenya zimeongezeka mara nne na kufikia 80. Ufaransa pia inashika nafasi ya pili kwa kutoa mikopo kwa Kenya katika msingi wa uhusiano baina ya nchi hizi mbili Ufaransa pia inashika nafasi ya nne kwa uwekaji vitega uchumi nchini Kenya.
Die Zeit
Huko huko nchini Kenya gazeti la Die Zeit linazungumzia juu ya suala la ukabila, katika makala yake gazeti hilo linasema ukabila una uzito mkubwa katika siasa, nchini Kenya na linaeleza. Makabila ndiyo yenye uzito mkubwa nchini Kenya na siyo vyama vya kisiasa. Lakini Kenya ni nchi iliyopiga hatua kubwa kimaendeleo barani Afrika. Ni nchi yenye tabaka la kati kubwa na watu wenye moyo wa ujasirimali. Hata hivyo nchini Kenya usasa bado unaenda sambamba na ukale. Gazeti hilo la Die Zeit limemnukulu mtaalamu wa masuala ya utamaduni nchini Kenya, Kimani Njogu akieleza kuwa ukabila ulipaliliwa na wakoloni.
Katika njama zao za kuzuia umoja wa Waafrika wakati huo wakoloni wa Kiingereza waliwatengansisha watu katika msingi wa makabila. Gazeti la Die Zeit linasema kila kabila lilitengewa sehemu yake, na kutokana na sera hiyo mipaka iliwekwa baina ya watu, na hivyo ndivyo msingi wa ukabila ulivyojengwa nchini Kenya. Hata hivyo katika kipindi cha kuelekea kwenye uhuru, ilionekana kana kwamba makabila yalihitajika ili kujiandaa kisiasa na hapo mwanzoni Wakikuyu na Wajaluo walishikana wakati wa kupigania uhuru. Lakini gazeti hilo linakumbusha katika makala yake kwamba njia ya kuelekea kwenye mamlaka ilisababisha mvutano baina ya makabila hayo. Gazeti la Die Zeit limemnukulu mtaalamu Kimani Njogu akisema ukabila ni njama inayotumika kudumisha mamlaka.
die tageszeitung
Katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo gazeti la die tageszeitung linatuarifu kwamba wafungwa kwenye jela moja hawataki kwenda nyumbani hata baada ya kumaliza kutumikia kifungo. Jee ni kwa nini? Gazeti hilo linatueleza kwamba katika jela ya Osio iliyoko karibu na jiji la Kisangani la kaskazini mashariki mwa Kongo ilijengwa na wakoloni wa Kibelgiji mnamo mwaka 1958.
Hata hivyo mkuu wa idara ya sheria katika jimbo la mashariki la Tshopo, Gerard Kombozi alishangazwa alipotambua kwamba wafungwa walikuwa wanakataa kuondoka. Uchunguzi ulibainisha kwamba karibu na jela hiyo wakaazi wameanza kuchimba almasi. Gazeti la die tageszeitung linasema baadhi ya wafungwa na walinzi waliungana na kujenga mji karibu na jela na wafungwa hao na walinzi wanafanya biashara ya madini katika mji huo kwa sababu wana uhuru wa kujisimamia wenyewe.
Bild Zeitung
Makala ya gazeti la Bild inatufahamisha juu ya aliyekuwa mcheza tennis maarufu duniani, Boris Becker wa Ujerumani na ajira yake mpya. Gazeti hilo linatufahamisha zaidi kwamba Jamhuri ya Afrika ya Kati imemwajiri Boris Becker kuwa balozi wake.
Becker pia anatarajiwa kuwa mwambata wa michezo na utamaduni kwenye Umoja wa Ulaya, na kutokana na uteuzi huo atakuwa na hadhi ya kidiplomasia. Becker amaeahidi kutumia mitandao yake ya kimataifa pamoja na mahusiano yake na watu mashuhuri ili kuisaidia Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Mwandishi: Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen
Mhariri:Josephat Charo