Afrika katika magazeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 26.08.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Mnamo wiki hii magazeti ya Ujerumani yameandika juu ya kutatizika kwa juhudi za kuleta amani nchini Sudan Kusini na juu ya kampeni ya kuyatokomeza maradhi ya homa ya manjano barani Afrika

Aliekuwa Makamu wa Rais wa Sudan Kusini Riek Machar

Aliekuwa Makamu wa Rais wa Sudan Kusini Riek Machar

Gazeti la "die tageszeitung" linasema juhudi za kuleta amani nchini Sudan Kusini zimezidi kutatizika baada ya aliekuwa Makamu wa Rais wa nchi hiyo Riek Machar kuikimbia nchi.

Gazeti hilo linaeleza kwamba Riek Machar aliekuwa hasimu mkubwa wa Rais Salva Kirr sasa yuko nchini Sudan, baada ya uadui wa wanasiasa hao wawili kuitumbukiza nchi yao,katika vita.

Machar alikimbia Sudan Kusini katikati ya mwezi wa Juni, baada ya kuondolewa kwenye wadhifa wake, na Rais Kiir. Aliondoka na kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa miguu na wafuasi wake. Gazeti la "die tageszeitung" limezikariri habari ambazo hazijathibitishwa zikisema kuwa Machar alikuwamo katika hali mbaya ya afya alipoenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Gazeti la "die tageszeitung" pia limeikariri taarifa ya gazeti moja la Kenya ikisema kuwa Sudan ilimpelekea Machar, ndege nchini Kongo ya kumsafirisha hadi Khartoum. Gazeti la "die tageszeitung" linasema kuwepo kwa Riek Machar nchini Sudan kutaipa serikali ya nchi hiyo turufu ya kushawishi mambo ya Sudan kusini.

Gazeti hilo linatilia maanani kwamba hata wakati wa harakati za ukombozi Riek Machar alikuwa anawania kujenga ushirika na Sudan ili kuweza kuukabili uzito wa waasi wa kabila la walio wengi la Dinka la Rais Salva Kirr.

Buhari awavunja moyo vijana

Vijana waandamana nchini Nigeria

Vijana waandamana nchini Nigeria

Gazeti la "Neues Deutschland" linasema katika makala yake kwamba Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria aliekuwa mwakilishi wa matumaini makubwa, amewavunja moyo vijana wa nchi yake.

Gazeti hilo linaeleza kwamba uchumi wa Nigeria,ambao ulikuwa unaongoza barani Afrika sasa unarudi nyuma, wakati idadi ya watu wasiokuwa na ajira inazidi kuongezeka. Thamani ya sarafu ya Nigeria, Naira pia inaendelea kushuka.Vijana wa nchi hiyo wanahisi kuwa wamewekwa kandoni mwa jamii.


Gazeti la "Neues Deutschland" linakumbusha kwamba vijana wengi walishiriki katika kupiga kura wakiwa na matumaini ya kuyabadilisha maisha yao. Vijana wa Nigeria walihisi kuwa na nguvu ya kuujenga mustakabal wao.

Hata hivyo gazeti la "Neues Deutschland" limemnukulu aliekuwa Waziri wa elimu Oby Ezekwesili akisema kwamba tangu aingie madarakani, Rais Buhari amekuwa anatawala kwa kutoa amri na kudhibiti kila kitu.

Waziri huyo amekaririwa na gazeti hilo akisema kwamba sera za Rais Buhari zimetoa mwanya wa kufanyika ufisadi na kusababisha uchumi uzorote kiasi kwamba taji la hapo awali la kuwa taifa kuu la kiuchumi barani Afrika limerejea tena Afrika Kusini.

Gazeti la "Neues Deutschland" limemnukulu Waziri huyo wa zamani,Ezekwesili akisema kuwa miezi 15 ya kwanza ya uongozi wa Rais Buhari imekuwa ya kuvunja moyo. Gazeti hilo linaongeza kusema, kwamba hata ahadi aliyoitoa ya kuutokomeza ugaidi wa kundi la Boko Haram bado hajaitimiza.

Mapambano dhidi ya homa ya manjano
Gazeti la "Süddeutsche" limeipa taarifa yake kichwa cha habari kinachosema sindano Milioni 10 zinahitajika. Gazeti hilo linaizungumzia kampeni kabambe ya kupambana na maradhi ya homa ya manjano barani Afrika kote. Lakini linasema zipo changamoto kadhaa.

Linaeleza kwamba muda unayoyoma na majira ya mvua yanapiga hodi. Na kama kawaida hakuna masika yasiyokuwa na mbu.! Mlipuko wa maradhi hayo ulioanza mnamo mwezi Desemba mwaka uliopita unaweza kuwa mkubwa zaidi.

Gazeti linasema sababu ni kwamba itakuwa vigumu kuwafikia watu wote katika majira hayo ya mvua.

Gazeti la "Süddeutsche" limemnukulu Mkurugenzi wa kitengo cha shirika la afya duniani,WHO , cha kuzuia magonjwa ya milipuko, Dr. Sylvie Briand akieleza kuwa lengo la kampeni hiyo ni kuuzuia mlipuko uliofumuka sasa.

Gazeti la " Süddeutsche" linafahamisha kwamba watu Milioni 14 watapewa chanjo katika wiki zijazo nchini Angola na katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo.

Gazeti hilo linasema kwa muda mrefu wataalamu wamekuwa wanatahadharisha juu ya hatari ya kulipuka kwa maradhi ya homa ya manjano katika miji mikubwa kama Kinshasa. Gazeti la "Südeutsche" linafahamisha kwamba maalfu ya watu barani Afrika wamekumbwa na maradhi hayo na zaidi ya 500 wameshakufa.

Mwandishi: Mtullya Abdu.

Mhariri: Mohammed Khelef