Afrika katika magazeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 19.08.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Magazeti ya Ujerumani yameandika juu ya ushindi wa Rais Edgar Lungu katika uchaguzi wa nchini Zambia.Gazeti la "Berliner linatahadharisha kwamba watu Milioni moja wamo hatarini kukumbwa na baa la njaa nchini Malawi.

Wafuasi wa Rais Edgar Lungu wakisherehekea nchini Zambia

Wafuasi wa Rais Edgar Lungu wakisherehekea nchini Zambia

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linatilia maanani kwamba Rais Edgar Lungu ameshinda uchaguzi nchini Zambia lakini matatizo yake sasa ndiyo yataanza.Mbali na malalamiko ya upande wa upinzani ,Lungu atakabiliwa na changamoto za kiuchumi.

Gazeti hilo linasema baada ya kushinda uchaguzi, Rais Lungu anapaswa kujibu swali: jee ni sera gani ya kiuchumi itakuwa sahihi kwa Zambia katika muktadha wa kuanguka kwa bei ya shaba, kuanguka kwa thamani ya sarafu ya nchi hiyo na kuongezeka kwa mfumuko wa bei.

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linaeleza kwamba ustawi wa uchumi nchini Zambia mnamo mwaka huu utafikia kiasi cha asimilia tatu,tofauti na miaka ya nyuma ambapo ustawi ulifikia hadi asilimia 10 kutokana na bei ya shaba kuwa nzuri wakati huo.

Kutokana na matumaini ya bei ya shaba kuwa nzuri Rais Edgar Lungu alitoa ahadi nyingi kwa wananchi wake. Jee atazitimza,ahadi hizo gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linauliza?

Milioni moja waathirika na ukame Malawi

Ukame waikumbuka Malawi vibaya sana

Ukame waikumbuka Malawi vibaya sana

Gazeti la "Berliner " linasema bara la Afrika linapitia kipindi kibaya sana cha ukame, na nchi iliyokumbwa zaidi na baa hilo ni Mawali. Gazeti hilo limezinukulu taarifa zinazosema kwamba watu Milioni moja wa nchi hiyo wamo katika hatari ya kukumbwa na janga la njaa.

Gazeti la "Berliner" linaeleza kuwa kilimo cha zao moja la mahindi, kinaifanya hali iwe mbaya zaidi. Gazeti hilo linasema hakuna tone hata moja la mvua lililodondoka katika msimu uliopaswa kuwa wa mvua.

Gazeti la "Berliner " linaeleza kuwa Malawi imo miongoni mwa nchi masikini duniani, na kwa hivyo haina akiba ya kuiwezesha kuimudu hali hiyo ya ukame. Kwa mujibu wa makisio, watu zaidi ya Milioni 7 watahitaji misaada ya mashirika ya kimataifa ili kuweza kuendelea kuishi.

Polio yarudi tena Afrika


Maradhi ya kupooza, polio, yamerejea tena barani Afrika.Hizo ni habari zilizochapishwa na gazeti la "Der Tagesspiegel" na linaizungumzia hai ya nchini Nigeria. Gazeti hilo linaeleza kwamba hali hiyo imesababishwa na mashambulio ya kigaidi yanayofanywa na magaidi wa Boko Haram.

Pamoja na kuwaweka watu roho juu kaskazini mashariki mwa nchi hiyo, magaidi wa Boko Haram pia wamesababisha maradhi ya polio yarejee nchini Nigeria. Mashambulio yao yamesababisha mazingira ya kustawisha virusi vya maradhi hayo na kuenea. Gazeti la "Der Tagesspiegel" limeinukulu taarifa ya Shirika la Afya duniani, WHO ikisema kuwa watoto wawili wamekumbwa na maradhi hayo katika jimbo la Borno la kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Gazeti hilo linasema wataalamu walikuwa na matumaini kwamba njia zote za maambukizi zilikuwa zimeondoshwa na kwamba hadi mwaka ujao bara lote la Afrika lilikuwa liondokane kabisa na ugonjwa huo.

Gazeti la "Der Tagesspiegel" limeeleza kwamba katika jimbo hilo la Borno, haikuwezekana kuwapa chanjo watoto nusu Milioni,katika kipindi cha miaka miwili iliyopita,kwa sababu magaidi wa Boko Haram walikuwa wanawashambulia maafisa waliokuwa wanatoa chanjo hizo.

Jee nchi za Ulaya zina haki ya kulalamika juu ya idadi kubwa ya wakimbizi wanaoingia katika nchi hizo. Gazeti la "Neues Deutschland" linajibu swali hilo kwa kulinganisha hali ya nchini Uganda na ya Ulaya.

Gazeti hilo linasema katika nusu ya kwanza ya mwaka huu Uganda ilipokea wakimbizi nusu Milioni kutoka Sudan Kusini, Burundi na kutoka nchi nyingine za jirani.

Gazeti la "Neues Deutschland" linatilia maanani kwamba Uganda ni nchi yenye wakaazi wapatao Milioni 40 na kipato cha wastani cha dola 626 kwa mwaka.Lakini licha ya hayo Uganda kwa sasa inawapa hifadhi wakimbizi Milioni moja na nusu kutoka nchi jirani.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen:

Mhariri: Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com