Afrika katika magazeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 28.06.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Magazeti ya Ujerumani wiki hii yameandika juu ya kukamatwa nchini Uingereza, kwa mkuu wa usalama wa Rwanda, Karenzi Karake na juu ya kuja juu kwa vyama vya upinzani nchini Afrika Kusini,kuhusu Rais Omar-al- Bashir

Rais Paul Kagame wa Ruanda

Rais Paul Kagame wa Rwanda

Gazeti la "die tageszeitung" limeandika juu ya kukamatwa nchini Uingereza kwa mkuu wa usalama wa Rwanda Jenerali Karenzi Karake. Jenerali huyo alikamatwa jijini London Jumamosi ya wiki iliyopita . Gazeti la "die tageszetung" linasema Jenarali Karake alikamatwa kwenye uwanja wa ndege wa Heathrow kutokana na hati ya kutatanisha ya kuwezesha kumkamata iliyotolewa na Uhispania.


Gazeti la "die tageszeitung" limeeleza kwamba maafisa wa usalama wa Uingereza walimtia ndani Jenerali Karenzi Karake kutokana na hati hiyo iliyotolewa na Uhispania kutokana na kwamba mnamo mwaka wa 2008 mwanasheria wa Uhispania alitoa amri ya kukamatwa maafisa 40 wa ngazi za juu wa jeshi la Rwanda kutokana na kutuhumiwa kuhusika na uhalifu nchini Rwanda na katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,ikiwa pamoja na mauaji ya raia tisa wa Uhispania.

Hata hivyo gazeti la "die tageszeitung" linasema tuhuma zilizotolewa na mwanasheria wa Uhispania zinatokana na kauli iliyotolewa na mtu mmoja anaeishi nje ya Afrika. Na pamoja na hayo ushahidi wake haujathibitishwa.

Wapinzani nchini Afrika Kusini wajaa juu kuhusu Rais al- Bashir


Gazeti la NZZ linalotolewa kila Jumapili wiki hii limeandika juu ya kadhia ya Rais wa Sudan Omar al -Bashir aliekuwapo nchini Afrika Kusini kuhudhuria mkutano wa viongozi wa nchi za Umoja wa Afrika. Wapinzani na wanaharakati kadhaa walitaka Bashir akamatwe ili kuitekeleza amri ya Mahakama ya Kimataifa ya mjini The Hague,ICC .Mahakama hiyo inamtuhumu Rais huyo wa Sudan kuhusika na uhalifu wa kivita.

Gazeti na NZZ linasema kutokana na Afrika Kusini kumwachia Rais Bashir aondoke nchini, Mahakama ya Kimataifa ya ICC imempoteza mshirika muhimu sana barani Afrika. Gazeti la NZZ limelinukuu tamko la chama kinachotawala nchini Afrika Kusini, ANC lililouhalalisha uamuzi wa kutomkamata Rais Bashir.

Chama hicho kimesema katika tamko lake kwamba uhalifu mkubwa unatendeka katika nchi ambazo siyo wanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya ICC na watuhumiwa hawaadhibiwi.Na gazeti la "die tageszeitung" limeripoti, kwamba wapinzani na wanasheria wamekuja juu kutaka serikali ya nchi yao ichunguzwe juu ya kadhia ya Rais Omar al-Bashir.

Gazeti la "Süddeutsche" limeandika juu ya madai kwamba wanajeshi wa Umoja wa Mataifa, na hasa Wafaransa ,wanaolinda amani katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, wamewadhalilisha watoto kingono. Gazeti hilo linasema yumkini uhalifu huo bado unaendelea .

Gazeti la "Süddeutsche" limeikariri taarifa ya gazeti la Uingereza ,"The Guardian" inayosema kuwa, askari 16 wa Umoja wa Mataifa walihusika na uhalifu huo kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na mjumbe wa Umoja wa Mataifa. Mjumbe huyo aliwasilisha taarifa ya uchunguzi wake kwa wakubwa zake lakini Umoja wa Mataifa haukuchukua hatua.

Tabaka la kati lastawi polepole barani Afrika
Gazeti la "Berliner " limeandika juu ya kutoweka kwa matumaini ya kampuni ya vyakula Nestle juu ya bara la Afrika. Meneja wa kampuni hiyo Paul Bulcke ameliambia gazeti la "Berliner" kwamba ,baada ya kulifungua tawi jipya la kampuni, yake nchini Angola, miaka 3 iliyopita matumaini yalikuwa makubwa.

Meneja huyo ameliambia gazeti la "Berliner" kwamba kampuni yake ilikuwa na matumaini ya kuuza bidhaa za zenye thamani ya dola Bilioni 6 barani Afrika, hadi kufikia mwaka wa 2020. Lakini Meneja huyo ameliambia gazeti la "Berliner" kwamba tabaka la kati lenye uwezo wa kifedha, halistawi haraka barani Afrika.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Iddi Ssessanga