Afrika katika magazeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 01.02.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Wiki hii magazeti ya Ujerumani yameandika juu ya mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika, mgogoro wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, na msimamo wa Ujerumani juu ya migogoro ya barani Afrika

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Ursula von der Leyen

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Ursula von der Leyen

Gazeti la "Berliner " limeandika juu ya mkutano wa kilele wa nchi za Umoja wa Afrika.Gazeti hilo linasema mkutano huo mjini Addis Ababa kwa mara nyingine umeonyesha jinsi Umoja huo ulivyolemewa na migogoro.

Gazeti la "Berliner " limemnukuu makamu wa Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Afrika , Erastus Mwencha akisema kwamba viongozi wa nchi za Afrika safari hii walidhamiria kusisitiza juu ya mafanikio ya bara lao ili kuiondoa picha mbaya inayosawiriwa juu ya Afrika.

Pamoja na matukio yanayoleta matumaini ni ustawi wa uchumi uliopo juu ya kiwango cha ustawi wa duniani kote,kupungua kwa mizozo ya kivita na kujengeka kwa tabaka la kati. Hata hivyo gazeti la "Berliner" linasema kwamba viongozi wa Afrika kwenye mkutano wa mjini Addis Ababa walirejerea katika ajenda za kale, yaani za migogoro kama vile katika Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Gazeti la "Berliner" pia limeikariri ripoti ya taasisi ya Afrika Kusini inayoshughulikia masuala ya usalama inayoonyesha kwamba nchi 26 za Afrika bado zimo katika hali tete. Gazeti hilo limetilia maanani, kwamba idadi hiyo inawakilisha tarkiban nusu ya nchi zote za bara la Afrika.

Ujerumani kusaidia kijeshi barani Afrika

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limearifu kwamba Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Ursula von der Leyen anakusudia kukaa kitako na waziri mwenzake, wa mambo ya nje Frank-Walter Steinmeier ili kujadiliana juu ya jinsi Ujerumani inavyoweza kusaidia kijeshi barani Afrika.

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" pia limefahamisha kwamba Waziri wa Ujerumani wa ushirikiano wa maendeleo,Gerd Müller pia atashirikishwa katika mashauriano hayo juu ya kuuweka mkakati wa Ujerumani juu ya Afrika.Waziri wa ulinzi wa Ujerumani von der Leyen amenukuliwa na gazeti la "Frankfurter Allgemeine" akisema kuwa Ujerumani inao wajibu wa kusaidia barani Afrika.

Jacob Zuma kukabiliwa na changamoto kubwa

Gazeti la "Süddeutsche" wiki hii linazungumzia juu ya changamoto inayoweza kumkabili Rais Jacob Zuma katika uchaguzi wa rais utakaofanyika nchini Afrika Kusini katika mwezi wa Aprili.

Gazeti hilo linasema kwamba wanawake wawili mashuhuri sana katika ulingo wa siasa wameungana ili kumpa Rais Zuma changamoto katika uchaguzi wa mwezi Aprili.Wanawake hao ni Helen Zille kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Afrika Kusini Democratic Alliance.Na mwengine ni aliekuwa mpinzani mkubwa wa ubaguzi Mamphela Ramphele atakaegombea urais kwa tiketi ya chama hicho cha Democratic Alliance kinachotambulika kuwa chama cha wazungu.

Gazeti la"Süddeutsche" limemnukuu Katibu Mkuu wa chama tawala cha Afrika Kusini ANC, Gwede Mantashe akisema kuwa chama cha DA sasa kinamkodi mtu mwenye sura nyeusi ili kukiwakilisha katika uchaguzi.Gazeti hilo limetilia maanani kwamba, katika miaka ya hivi karibuni watu waliokuwa wanakiunga mkono chama cha ANC sasa wanakipa kisogo chama hicho

.Kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni, ni asilimia 53 tu ya watu nchini Afrika Kusini watakaokipigia kura chama cha ANC. Katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2009 asilimia 65,9 ya watu walikipa kura zao chama cha ANC.

Kesi ya Rwabukombe yasikilizwa Ujerumani

Gazeti la "die tageszeitung" wiki hii limeripoti juu ya kesi inayomkabili aliekuwa meya wa mji wa Mavumba, nchini Rwanda, Onesphere Rwabukombe. Gazeti hilo linafahamisha kwamba Mahakama ya mjini Frankfurt ,Ujerumani, imehukumu kesi ya kwanza ya mauaji halaiki yaliyofanyika nchini Rwanda. Mshtakiwa ni Onesphore Rwabukombe, mwananchi wa Rwanda anaeishi nchini Ujerumani.

Mwendesha mashtaka anataka Rwabukombe apewe adhabu ya kifungo cha maisha jela kwa kuhusika na mauaji halaiki ya watu 1200 kwenye kanisa moja katika kijiji cha Kiziguro nchini Rwanda.Gazeti la die " tageszeitung" limetufahamisha kwamba hukumu itatolewa tarehe 18 mwezi huu.

Mwandishi:Mtullya Abdu./Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Yusuf Saumu