1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Abdu Said Mtullya12 Januari 2014

Magazeti ya Ujerumani wiki hii yameandika juu ya migogoro ya Sudan Kusini,Jamhuri ya Afrika ya Kati na juu ya wakimbizi kutoka Afrika walioko nchini Israel.

https://p.dw.com/p/1ApGl
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter SteinmeierPicha: DW/B. Riegert

Juu ya mgogoro wa Sudan Kusini gazeti la "Süddeutsche Zeitung" limearifu juu ya uwezekano wa majeshi ya Ujerumani kupelekwa katika nchi hiyo ili kuwalinda raia.

Hata hivyo gazeti hilo la "Suddeutsche" limetoa ufafanuzi kwa kumnukuu waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier.Waziri Steinmeier ameliunga mkono azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa juu ya kupeleka majeshi katika Sudan Kusini.

Bwana Steinmeier amekaririwa na gazeti hilo akisema kwamba jumuiya ya kimataifa inachukua hatua za kujaribu kuleta amani katika Sudan Kusini.Waziri huyo amesema, kwamba kwa upande wake Ujerumani inatoa misaada ya kibinadamu. Gazeti la "Süddeutsche Zeitung"limetilia maanani kwamba Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani hakutoa kauli thabiti juu ya kushiriki kwa majeshi ya nchi yake katika mgogoro wa Sudan Kusini.

Jamhuri ya Afrika ya Kati

Gazezi la "Frankfurter Allgemeine"limechapisha makala juu ya mgogoro wa Jamhuri ya Afrika ya Kati. Gazeti hilo limemnukuu Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa akisema kuwa nchi yake haitaongeza idadi ya wanajeshi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. Waziri Laurent Fabius amesema kuwa hali ni ngumu katika nchi hiyo.

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limeripoti kwamba hatua za kuyanyang'anya silaha makundi yanayopigana zinasonga mbele pole pole sana. Ufaransa imewapeleka askari wake 1300 katika Jamhuri ya Afrika ya Kati na wataendelea kuwepo huko mpaka utakapopitishwa uamuzi mwingine. Gazeti la"Frankfurter Allgemeine" limefahamisha kwamba Ufaransa ilikuwa na mpango wa kuwapeleka jumla ya askari 1600 katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Umoja wa Ulaya.

Wakati mazungumzo yanafanyika juu ya kuutatua mgogoro wa Jamhuri ya Afrika ya Kati,Umoja wa Ulaya unatafakari kupeleka askari. Gazeti la "die tageszeitung" limearifu kwamba kikosi cha askari hadi 1000 kutoka nchi za Umoja wa Ulaya kinaweza kupelekwa katika nchi hiyo ya Afrika ya kati ili kuwapokea mzigo askari wa Ufaransa ambao tayari wako katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Waafrika wakwama Israel

Gazeti la "Der Tagesspiegel" linayazungumzia matatizo ya maalfu wa Waafrika waliokwama nchini Israel. Gazeti hilo limearifu kwamba maalfu ya Waafrika hao wamekuwa wanaandamana kwa siku kadhaa ili kudai haki ya kutambuliwa kuwa ni wakimbizi.Gazeti la "Der Tagesspiegel" limeripoti kwamba Waafrika hao kutoka Sudan Kusini, Ethiopia na Eritrea wanataka wapewe haki ya kuishi nchini Israel.

Waafrika 53,000 kutoka nchi hizo hawana mpango wa kurejea katika nchi zao.Lakini gazeti la "Der Tagesspiegel" limefahamisha kwamba serikali ya Israel inadhamiria kuwafukuza Waafrika hao. Na ili kuihamasisha jumuiya ya kimataifa juu ya matatizo yao Waafrika hao wamefanya maandamano katika miji ya Tel Aviv,Eilat na Jerusalem.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman