Afrika katika magazeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 08.09.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Wiki hii magazeti ya Ujerumani yameandika juu ya uamuzi wa wabunge wa Kenya wa kuiondoa nchi yao kutoka Mahakama ya Kimataifa ya mjini The Hague,ICC, juu ya Mashariki mwa Kongo na juu ya Madiba

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na Makamu wake William Ruto

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na Makamu wake William Ruto

Gazeti la "die tageszeitung" limechapisha makala juu ya uamuzi wa wabunge wa Kenya wa kuitoa nchi yao kwenye Mahakama ya Kimataifa ya mjini the Hague ICC, kwa usemi mwingine kujitoa kwenye mkataba wa sheria za Rome.

Gazeti hilo linaeleza kuwa wabunge hao wameupitisha uamuzi wao wakati Rais wao Uhuru Kenyatta na makamu wake William Ruto wanatarajiwa kufunguliwa kesi kwenye mahakama ya mjini The Hague. Kesi ya makamu wa Rais, inatarajiwa kuanza tarehe 10 mwezi huu wakati ile ya Rais Kenyatta imepengwa kuanza tarehe 12 mwezi wa Novemba. Wanasiasa hao wanakabiliwa na mashtaka ya kutenda uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Mashtaka ya uhalifu dhidi ya ubinadamu

Mashitaka hayo yanafuatia mauaji yaliyotokea baada ya uchaguzi mwishoni mwa mwaka wa 2007. Watu 1300 walikufa kutokana na mapigano baina ya makabila mbalimbali. Kenyatta na Ruto wanadaiwa kwamba waliyachochea makundi ya wanamgambo miongoni mwa makabila yao ya wakikuyu na wakalenjin.

Gazeti la "die tageszeitung" linatilia maanani katika makala yake kwamba uamuzi wa wabunge wa Kenya hautawaepusha Rais Kenyatta na makamu wake Ruto kufanyiwa kesi. Hata hivyo gazeti hilo limemkariri mwasisi wa mswada uliowasilishwa na wabunge Bwana Asman Kamama akisema kuwa uamuzi huo utapokewa vizuri barani Afrika kote. Bwana Kamama pia amekaririwa akisema kwamba,Marekani, China na Urusi hazimo katika ICC, sasa kwa nini Afrika iwemo?

Ukatili mashariki mwa Kongo:watu wazikwa hai
Gazeti la "Die Welt" limechapisha makala juu ya hali ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Linaarifu katika makala hiyo kwamba majeshi ya Umoja wa Mataifa yamewatimua waasi wa M23. Baada ya kukunja mikono nyuma kwa muda wa miaka mingi,sasa majeshi hayo yanaingia katika mapambano dhidi ya waasi.

Gazeti la "Die Welt" limemnukulu mwakilishi wa wakfu wa Ujerumani Hanns-Seidel bwana Götz Heinicke akisema kuwa ukatili unaofanywa na waasi mashariki mwa Kongo hauna mfano .Amesema watu wanazikwa wangali hai. Bwana Heinicke ameliambia gazeti la "Die Welt" kuwa alipewa taarifa kwamba katika hospitali moja amelazwa mama mmoja,anaetibiwa baada ya kumwagiwa petroli katika sehemu zake za siri na kuchomwa moto na waasi.

Mwakilishi huyo wa Wakfu wa Ujerumani nchini Kongo Bwana Heinicke amenukuliwa na gazeti la "Die Welt "akisema kwamba unyama mkubwa unafanyika mashariki mwa Jamhuri ya Kongo.

Madiba augulia nyumbani

Rais mstaafu wa Afrika Kusini,Nelson Mandela ametoka hospitali na kurejea nyumbani.Hizo ni bahari zilizoandikwa na gazeti la "Der Tagesspiegel" Lakini gazeti hilo limefahamisha kwamba Mandela alitolewa hospitali kutokana na maombi ya familia yake. Gazeti la "Der Tagesespiegel" limefahamisha kwamba nyumba ya Mandela imetayarishwa ili kuweza kuyakidhi mahitaji yote kihospitali.

Ndovu 30,000 wauliwa katika Afrika ya Kati

Gazeti la "Frankfurter Rundschau"linatahadharisha juu ya hatari ya kutoweka kwa ndovu duniani. Gazeti hilo linakumbusha kwamba palikuwapo enzi ambapo lilikuwa jambo la kufurahisha kuwaona ndovu,viumbe wakubwa,wenye nguvu,na wenye kuogopewa. Lakini enzi hiyo sasa haipo tena. Gazeti la "Frankfurter Rundschau" linaeleza kwa nini: mwaka jana pekee,ndovu 30,000 waliuawa barani Afrika na hasa katika misitu ya Kongo. Sababu ya kuuliwa kwa viumbe hao ni pembe zao

Mkurugenzi wa shirikisho la bustani za wanyama duniani,WAZA Jörg Junhold amesema ujangili wa ndovu umefikia kiwango cha kutisha. Bwana Junhold ameliambia gazeti la "Frankfurter Rundschau" kwamba kutoweka kwa maskani ya wanyama hao pamoja na ujangili ni mambo yanayochangia katika kuuhatarisha uhai wa viumbe hao.Mkurugenzi huyo bwana Juhhold amesema uhai wa tembo umo katika mikono ya binadamu

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Yusuf Saumu