1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Angela Mdungu (Mhariri: Bruce Amani)
19 Aprili 2024

Yafahamu yaliyoandikwa katika magazeti ya Ujerumani wiki hii. Moja kati ya hayo ni kuhusu hali mbaya ya kiutu Sudan, baada ya mwaka mmoja wa vita.

https://p.dw.com/p/4exz7
Kongamano la kuisaidia Sudan lilifanyika Paris Ufaransa
Moshi ukifuka Sudan baada ya mashambuliziPicha: Marwan Ali/AP/dpa/picture alliance

Frankfurter Allgemeine

Gazeti la Frankfurter Algemeine wiki hii, liliandika kuhusu namna Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, alivyowapongeza wanajeshi kwa mchango wao katika amani na usalama kwenye ukanda wa Sahel. Gazeti hili limemnukuu Kansela Scholz akisema ”Miaka 10 iliyopita, Mali ilikuwa hatarini kusambaratika, magaidi wenye itikadi kali za Kiislamu na watu wanaotaka kujitenga walitishia kuteka mji mmoja baada ya mwingin nchini Mali."

Scholz aliongeza kuwa kitendo cha wanajeshi hao kuitumia nafasi hiyo kufanya juhudi za kuleta amani na kuilinda nchi na watu wake wakati huo lilikuwa jambo sahihi. Lakini kwa mujibu wa Scholz, uhuru wa watu kufanya shughuli zao unapozuiliwa, na na hali ya kisiasa inapofanya mazingira yawe magumu kwa walinda amani kuendelea kutimiza majukumu yao, ujumbe huo wa kulinda amani hauna budi kusitisha shughuli zao.

Frankfurter Allgemeine

Gazeti hilo hilo la Frankfurter Allgemeine liliandika pia kuhusu siasa za Senegal. Gazeti hilo linaeleza kuwa kuna mwamko mkubwa Senegal. Wanasiasa wawili wa upinzani waliokuwa gerezani siku chache kabla ya uchaguzi sasa wanaiongoza nchi. Mwanasiasa maarufu Ousmane Sonko hakuruhusiwa kugombea Urais. Mshirika wake wa karibu Bassirou Diomaye Faye aliwania kiti hicho badala yake, na kushinda katika duru ya kwanza ya uchaguzi kisha akamchagua Sonko kuwa Waziri Mkuu.

Bassirou Diomaye akihutubia baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Senegal 02.04.2024
Rais wa Senegal Bassirou Diomaye FayePicha: John Wessels/AFP

Gazeti hilo linatanabaisha kuwa, hatua yenyewe ya uchaguzi kufanyika nchini humo ni jambo linaloleta matumaini.  Rais aliyemaliza muda wake Macky Sall alionesha ustadi katika kuendeleza ushawishi wake hadi kufikia hatua ya kuahirisha uchaguzi baada ya mhula wake kumalizika.  Zaidi ya hapo, vijana wa Kisenegali walioamua kuandamana kupinga hatua hiyo hasa wanaounga mkono upinzani walikamatwa.

Lakini mwisho wa siku demokrasia ilishinda, na sasa kuna matumaini mapya kuwa Faye na Sonko watakuwa waasisi wa wanasiasa vijana wa kizazi kipya barani Afrika. Hasa magharibi na katikati mwa Afrika ambako marais wenye umri mkubwa wanang'ang'ania madaraka bila hofu.

Kwa ujumla, mabadiliko ya kizazi kimoja kwenda kingine katika bara hilo changa zaidi duniani bado hayajapiga hatua kubwa. Rais wa Nigeria Bola Tinubu ana miaka 72. Rais wa Afrika ya Kusini Cyril Ramaphosa mwenye miaka 71, pasi na shaka atasalia madarakani  baada ya  uchaguzi wa mwezi Mei. Frankfurter Allgemeine linakwenda mbali zaidi kueleza kuwa, watawala kama Museveni wa Uganda wanauona urais kama kazi ya maisha yao yote na kuandaa watakaoendeleza kazi zao kwa ajili ya kizazi kinachofuata. Na watu hao ni kutoka ndani ya familia.

die tageszeitung

Karibu magazeti yote yaliyotufikia wiki hii yaliandika kuhusu mwaka mmoja wa vita vya Sudan. die tageszeitung liliuangazia msaada ulioahidiwa na nchi wafadhili kwa ajili ya taifa hilo katika kongamano lililofanyika nchini Ufaransa. Gazeti hilo linaeleza kuwa, licha ya wahisani kuahidi fedha nyingi mjini Paris kwa ajili ya kuisaidia Sudan kupitia Umoja wa Mataifa,  namna ya kumaliza vita nchini humo bado ni kitendawili.

die tageszeitung linaarifu kuwa, mwanzoni mwa kongamano hilo, tume ya Umoja wa Ulaya iliahidi kutoa euro milioni 215 kwa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Sudan na euro nyingine milioni 140 kwa ajili ya kukabiliana na athari za mzozo huo katika mataifa Jirani.  Ujerumani nayo kulingana na Waziri wa mambo ya kigeni Annalena Baerbock, iliahidi euro 244 kwa ajili ya masuala hayo mawili. Ufaransa ilitoa ahadi ya euro milioni 110 na Marekani iliahidi kiasi saw ana Euro milioni 138. 

Mwanzoni mwa kongamano hilo, Jumla ya euro milioni 840 zilitarajiwa kupatikana na kuvuka lengo lililokusudiwa kupatikana kwa ajili ya Sudan.  Hayo yanajiri wakati Sudan ikitimiza mwaka mmoja tangu kuibuka kwa mpigano kati ya jeshi rasmi la serikali na Kikosi  cha RSF. Vita hivyo tayari vimeshasababisha mgogoro mkubwa wa kiutu na zaidi ya watu milioni 8 kuyahama makazi yao.

Kulingana na takwimu mpya zilizotolewa na Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ufaransa  Stéphane Séjourné;  watu milioni 27 nchini Sudan, wanategemea misaada na milioni 18 wana uhitaji mkubwa wa chakula. Na kwa maneno yake mwenyewe, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ujerumani Annalerna Baerbock amekiri kuwa vita vya Sudan, vimesababisha kutokea kwa mgogoro mkubwa zaidi wa wakimbizi duniani.


Süddeutsche Zeitung

Kuhusu vita hivyo vya Sudan, Süddeutsche Zeitung liliandika, kwa mwaka mmoja sasa, majenerali wawili wameendelea kuiangamiza Sudan bila mtu yeyote kuwazuia. Maisha yamekuwa machungu kwa zaidi ya watu milioni 25 nchini humo.

Kongamano la kuisaidia Sudan lilifanyika Paris, Ufaransa April 15, 2024
Wawakilishi wa mataifa wanachama katika kongamano la kuisaidia Sudan na mataifa jiraniPicha: Sarah Meyssonnier/REUTERS

Siku ya kwanza milipuko ya mabomu ilipoanza kusikika Kharthoum, jeshi liliamini kuwa litapata ushindi. Redio zilitangaza kauli ya juu kutoka jeshini kuwa maadui hawakuwa na nafasi. Ujumbe huu ulikuwa kana kwamba jeshi chini ya Jenerali Abdel Fattah al-Burhan lisingechukua muda mrefu kushinda.

Hata hivyo mambo yamekuwa tofauti. Mwaka mmoja baada ya kuibuka kwa mapigano Sudan, jeshi halina dalili ya kupata ushindi. Kundi hasimu la RSF linaonekana kuwa na dhamira kuu na kiongozi wake Mohammed Dagalo anatafuta muda muafaka. Dagalo analiongoza kundi hilo lililojizatiti vyema ardhini ambalo kipindi cha nyuma lilikuwa chini ya Omar al Bashir.

Süddeutsche Zeitung linamnukuu mtaalamu wa siasa za pembe ya Afrika Alan Boswell anayetahadharisha kuwa Sudan inaelekea kuangamia. Majenerali wawili hasimu wanaharibu kila kitu. Uchumi umeharibiwa, karibu miundombinu yote imeharibiwa kwa kiasi kikubwa. Kila mmoja, Burhani na Daglo walidhani watashinda lakini walikosea kwani hakuna upande unaoweza kuibuka mshindi katika vita hivi. Sudan inakabiliwa na kitisho cha mgawanyiko kati ya mashariki na magharibi kwa sababu siku hadi siku makundi ya wanamgambo yanayotokana na makundi ya kikabila yanaanzishwa na kuwa washirika wa pande hizo mbili hasimu.

Chanzo: Deutsche Zeitungen