AFISMA kugeuka Kikosi cha Kimataifa cha Amani | Matukio ya Afrika | DW | 01.03.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

AFISMA kugeuka Kikosi cha Kimataifa cha Amani

Viongozi wa jumuia ya ushirikiano wa kiuchumi Afrika magharibi-ECOWAS wameshauri kikosi cha Afrika cha AFISMA kigeuzwe haraka kuwa kikosi cha kimataifa cha kulinda amani nchini Mali ili kuweza kukigharimia.

Viongozi wa ECOWAS waakutana Yamoussoukro

Viongozi wa ECOWAS waakutana Yamoussoukro

Wakikutana katika mji mkuu wa Côte d'Ivoire,Yamoussoukro,marais wa mataifa ya Afrika Magharibi-wanachama wa jumuia ya ushirikiano wa kiuchumi-ECOWAS wameunga mkono miito iliyotolewa na Ufaransa iliyotuma wanajeshi zaidi ya elfu nne tangu januari mwaka huu,Marekani na serikali ya mjini Bamako kutaka kikosi cha AFISMA kigeuzwe kuwa cha kimakataifa cha kulinda amani nchini Mali.

Hiyo isiwe sababu ya kusahau opereshini zinazoendelea" amesema mwenyekiti wa halmashauri ya ECOWAS Kadré Desiré Ouadraogo."Ni kidokezo tu kinachoashiria pindi amani ikirejea,tutahitaji msaada wa Umoja wa mataifa wa hali na Mali."Amesema,Desiré Ouadraogo mwisho mwa mkutano wao wa siku mbili wa kilele mjini Yamoussoukro.

Thuluthi mbili ya wanajeshi elfu nane wa kikosi cha nchi za Afrika-AFISMA wamewekwa nchini Mali.

Wengi wao hawana bado uwezo wa kushiriki katika opereshini za kivita kwa hivyo wamesalia kusini mwa Mali na kuwaacha wanajeshi wa Ufaransa na wengine takriban elfu mbili wa Tchad walinde usalama wa miji ya kaskazini na kuwatimuwa pia wanamgambo wa kiislam waliojificha katika misitu na katika maeneo ya milimani-kaskazini ya Mali.

Gharama zitaongezeka

Viele Tote nach Kämpfen in Mali

Mapigano kati ya wanajeshi wa Ufaransa wakishirikiana na wale wa Mali dhidi ya wanamgambo wa kiislam huko Gao

Baada ya miezi kadhaa ya kuomba misaada ya kimataifa,wafadhili waliridhia hatimae walipokutana mwezi january mwaka huu mjini Addis Ababa kutenga dala laki nne na 55 elfu kwaajili ya Mali.

Kutokana na idadi ya wanajeshi kuongezeka zaidi ya mara dufu tangu walipoanza kupelekwa nchini Mali,jumuia ya ECOWAS inaamini gharama za shughuli hizo zitaongozeka na kufikia karibu dala bilioni moja mwaka huu.

Mpango wa kukigeuza kikosi cha AFISMA kuwa kikosi cha kimataifa cha kulinda amani utapelekea kutolewa fedha na shirika la Umoja wa mataifa linalosimamia shughuli za kulinda amani na kurahisisha kutolewaa ndege ambazo ni muhimu katika kuwasafirisha wanajeshi hadi katika eneo la kaskazini la Mali.

Hata hivyo baraza la Usalama la Umoja wa mataifa litabidi kwanza liuidhinishe mpango huo.Jumatano iliyopita,mwakilishi wa kudumu wa Ufaransa katika baraza la Usalama alisema taasisi hiyo muhimu ya kimataifa itamuomba katibu mkuu Ban Ki-Moon aripoti hadi kati kati ya mwezi huu kuhusu uwezekano wa kuundwa kikosi cha kimataifa cha kulinda amani nchini Mali.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP

Mhariri:Yusuf Saumu

DW inapendekeza