1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afisa mkuu wa riadha Kenya apigwa marufuku

23 Februari 2016

Shirikisho la riadha duniani - IAAF, limempiga marufuku mwenyekiti mtendaji wa shirikisho la riadha la Kenya – Athletics Kenya Isaac Mwangi kwa siku 180.

https://p.dw.com/p/1I0H2
IAAF Logo Monaco Zentrale
Picha: picture-alliance/dpa/S.Nogier

Mwangi anatuhumiwa kwa kuwaitisha hongo wanariadha wawili waliopatikana na hatia ya kutumia dawa ya kuongeza misuli nguvu ili kupunguza kipindi cha marufuku yao, madai ambayo Mwangi anayakanusha.

Hivi karibuni mwenyekiti huyo mtendaji wa AK aliwasilisha ombi la kujiuzulu kwa siku 21 ili kuwezesha uchunguzi huru kufanywa dhidi yake.

Hatua iliyochukuliwa na kamati ya maadili ya IAAF ina maana kuwa Mwangi hatakuwa na mchango wowote katika mashindano yoyote ya riadha ikiwemo michezo ya olimpiki itakayofanyika Rio de Janeiro, nchini Brazil mwaka huu.

Mwangi alijipata matatani baada ya wanariadha wawili Joy Sakari na Francisca Koki Manunga kudai kuwa aliwaitisha hongo ya karibu dola 50,000 ili kupunguza adhabu yao.

Wanariadha hao wawili walipatikana na hatia ya kutumia dawa za kuongeza misuli nguvu katika mashindano ya riadha duniani yaliyofanyika Beijing, China.

Mwanfishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Sekione Kitojo