1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afghanistan yatangaza timu itakayokutana na Taliban

Lilian Mtono
28 Machi 2020

Serikali ya Afghanistan imetangaza timu ya wajumbe 21 itakayoshiriki mazungumzo na Taliban, katika kile kinachotajwa kama ishara ya kupigwa hatua kwa mazungumyo hayo ya amani yanayosimamiwa na Marekani

https://p.dw.com/p/3a9rA
Doha  Intra Afghan Dialogue Afghanistan Konferenz
Picha: Getty Images/AFP/K. Jaafar

Timu hiyo iliyotangazwa Alhamisi (27.03.2020) na taasisi maalumu ya kitaifa inayoshughulikia amani, inaongozwa na mkuu wa zamani wa taasisi ya usalama na mfuasi wa rais Ashraf Ghani, Masoom Stanekzai na imejumuisha wanasiasa, maafisa wa zamani na wawakilishi wa vyama vya kiraia. Watano miongoni mwao ni wanawake.

Haikujulikana mara moja iwapo mpinzani wa kisiasa wa rais Ghani, Abdullah Abdullah pia atataja timu ya wajumbe walioteuliwa, ambayo wanadiplomasia wamesema itakuwa muhimu kwa kuzingatia ushawishi wa upande wake katika sehemu kubwa ya kaskazini na magharibi mwa nchi hiyo.

Kufuatia uteuzi huo wa wajumbe wa upande wa serikali kwenye mazungumzo hayo, hatua inayofuata itakuwa ni kuanza kwa mazungumzo na Taliban kama sehemu za mchakato unaolenga kuvifikisha mwisho vita vya muda mrefu ambavyo Marekani imejihusisha navyo na hatimaye kurejesha amani nchini humo.

Abdullah lehnt Ghanis Wiederwahl ab und kündigt eine Parallelregierung in Afghanistan an
Haijafahamika kama Abdullah ni mmoja wa wanachamaPicha: imago images/Xinhua

Msemaji wa Abdullah alisema huenda atathibitisha ama la kuhusu iwapo Abdullah alikuwa anakubaliana na timu hiyo.

Vyanzo viwili, cha kwanza ni mwanadiplomasia aliyeko mjini Kabul aliyezungumzia kwa kifupi suala hilo na kingine ambacho ni mjumbe wa timu ya Abdullah, aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina aliyesema mazungumzo yamekuwa yakiendelea na kuna uwezekano kwamba anaikubali timu hiyo ya serikali.

Marekani ilisaini makubaliano na Taliban ya kuondoa wanajeshi wake nchini Afghanistan mnamo mwezi Februari, lakini kumekuwepo na ucheleweshwaji kuelekea makubaliano kati ya serikali ya Afghanistan na kundi hilo la wanamgambo la Taliban, kwa sehemu kutokana na mvutano wa kisiasa kati ya rais Ghani na Abdullah, ambao kwa pamoja walidai kuwa viongozi halali wa Afghanistan baada ya uchaguzi uliozozaniwa ambao ulifanyika Septemba mwaka jana.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Mike Pompeo alishindwa kuwapatanisha viongozi hao wawili ili kuanzisha serikali ya umoja wa kitaifa wakati wa ziara iliyochukua siku nzima mnamo siku ya Jumatatu mjini Kabul, na kutangaza kuondoa msaada wa dola bilioni 1, kati ya misaada inayoitoa nchini Afghanistan, ambayo alisema hata hivyo hatua hiyo inaweza kuangaziwa upya.