Zidane: CR7 haondoki Real Madrid | Michezo | DW | 08.01.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Zidane: CR7 haondoki Real Madrid

Kocha mpya wa miamba wa Uhispania Real Madrid Mfaransa Zinedine Zidane ameonya kuwa mshambuliaji nyota Cristiano Ronaldo maarufu kama CR7 hataondoka klabu hiyo chini ya uongozi wake

Zidane amesema CR7 ndio roho ya Real Madrid na atafanya kila kitu kumsaidia ajiskie mwenye furaha. Kulikuwa na fununu kuwa Mreno huyo atakayefikisha umri wa miaka 31 mwezi ujao alishindwa kuelewana na kocha aliyeondoka Rafa Benitez.

Zidane anachukua usukani wa Real Madrid kwa mara ya kwanza wakati Deportivo la Coruna watakapowatembelea vijana wake katika ngome yao ya Santiago Bernabeu ambayo itafurika hadi pomoni baada ya kununuliwa tikiti zote za mchuano huu wa leo usiku.

Zidane ambaye alichukua nafasi ya Rafa Benitez aliyetimuliwa baada ya kuhudumu kwa miezi saba pekee, anapendwa sana na mashabiki wa Bernabeu kutokana na miaka yake mitano aliyokuwa pale kama mchezaji na hasa goli muhimu la ushindi alilofunga kazika fainali ya Champions League mwaka wa 2002.

Shirikisho la kandanda la Uhispania limemfungia mshambuliaji wa BARCELONA Luis Suarez kucheza michuano miwili ya Kombe la mfalme – Copa del Rey, kwa kuwatukana mahimu wao Espanyol.

Ripoti ya refarii ya mchuano huo uliokuwa na hisia kali uwanjani Camp Nou ambao Barca walishinda 4-1 Jumatano usiku, imesema Suarez aliwatukana wachezaji wa Espanyol kwenye handaki la kutoka vyumba vya kubadilisha jezi na kuingia uwanjani baada ya mchuano. Wachezaji wawili wa Espanyol walipewa kadi nyekundu wakati wa mchuano huo. Barcelona imesema itakata rufaa kuhusiana na hukumu hiyo, ikikanusha kuwa Suarez aliwatukana wapinzani wake. Mchuano wa marudiano utakuwa wiki ijayo nyumbani kwa Espanyol

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Iddi Sessanga

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com