1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Zelenskiy: Urusi inakishikilia mateka kinu cha Zaporizhzia

28 Machi 2023

Rais wa nchi hiyo Volodymyr Zelensky amesema wanajeshi wa Urusi wanakishikilia mateka kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia na kwamba usalama wake hautaweza kuhakikishwa hadi pale watakapoondoka eneo hilo.

https://p.dw.com/p/4PMfD
Ukraine Saporischschja | Präsident Wolodymyr Selenskyj & UN-Atomenergiechef Rafael Grossi
Picha: Efrem Lukatsky/AP Photo/picture alliance

Rais Zelensky ameitoa kauli hiyo mara tu baada ya kukukutana kwa mazungumzo na Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Kudhibiti Matumizi ya Nishati ya Nyuklia (IAEA) Rafael Grossi, katika kituo cha umeme kinachotumia nguvu ya maji cha Dnipro kaskazini mashariki mwa kinu cha nyuklia cha Zaporizhia.

Wanajeshi wa Urusi walichukua udhibiti wa kinu kikubwa zaidi cha nyuklia barani Ulaya tangu wiki za mwanzo za uvamizi wao nchini Ukraine na wamekuwa wakionyesha kutokuwa na dhamira ya kuondoka eneo hilo.

Katika hotuba yake ya video ya kila usiku,  Rais Volodymyr Zelenskiy amesema hakika ni jambo baya mno kuona kinu kikubwa zaidi cha nyuklia kikishikiliwa mateka kwa zaidi ya mwaka mmoja na kwamba hilo ni jambo baya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya nyuklia barani Ulaya na hata duniani kote.

Ukraine | Videoansprache von Präsident Selenskyj
Rais wa Ukraine, Volodymyr ZelenskiyPicha: Presidential Office of Ukraine

Aidha Zelensky amelaani pia mashambulizi ya Urusi huko Zaporizhia:

" Leo huko Zaporizhzhia, nilitembelea mahali ambapo makombora ya Urusi yalipiga  majengo ya makazi. Nyumba zimeteketea kwa moto na kuharibiwa vibaya. Makumi ya watu walijeruhiwa kufuatia mashambulizi haya mabaya ya Urusi. Magaidi hao walijua vyema ni wapi walikuwa wakielekeza makombora yao. Watu 37 wamejeruhiwa na wawili wamekufa. Zaidi ya watu 400 waliomba msaada. Rambirambi zangu kwa wale waliopoteza wapendwa wao. "

Soma pia: Urusi yaimarisha mzingiro dhidi ya Bakhmut, Ukraine yaapa kuulinda mji huo

Urusi na Ukraine wamekuwa wakishutumiana kufanya mashambulizi karibu na kinu hicho cha nyuklia na Mkuu wa IAEA amekuwa mara kadhaa akitoa wito wa kuwepo eneo lenye usalama karibu na Zaporizhia, na amejaribu kujadili na pande zote mbili bila mafanikio.

Mapigano yaendelea karibu na Bakhmut

Videostill | DW TV | Zerstörte Gebäude in Avdiivka
Eneo lililoshambuliwa huko Avdiivka, Ukraine.Picha: DW

Kwenye uwanja wa vita, vikosi vya Urusi vinaonekana kuelekeza nguvu zao katika mji wa Avdiivka, takriban kilomita 90 kusini mwa mji wa Bakhmut. Wizara ya Ulinzi ya Uingereza imesema katika taarifa yake ya kila siku juu ya vita hivyo kuwa Urusi imepata hasara kubwa katika uvamizi wake huko Avdiivka.

Soma pia: Mkuu wa IAEA kuelekea Urusi kwa mazungumzo kuhusu Ukraine

Wakati huo huo, mamlaka ya Ukraine imesema vikosi vyake vya ulinzi wa anga vilidungua jana Jumatatu ndege 12 zisizo na rubani karibu na mji mkuu Kyiv.

Hii leo Belarus imesema itazipokea silaha za nyuklia za Urusi kutokana na kile ilichokiita 'shinikizo lisilo na kifani' la Mataifa ya Magharibi, huku ikisisitiza kuwa kufanya hivyo hakukiuki makubaliano yoyote ya kimataifa.