1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya watu 300 wakamatwa baada ya kuandamana, Kenya

Admin.WagnerD20 Julai 2023

Maandamano ya upinzani nchini Kenya ya kuishinikiza serikali kubadilisha sheria za fedha yameingia siku yake ya pili kwa wiki hii. Zaidi ya watu 300 wamekamatwa baada ya kushiriki kwenye maandamano hayo jana Jumanne.

https://p.dw.com/p/4UABM
Kumekuwepo na maandamano ya kila mara tangu serikali ya rais William Ruto ilipoingia madarakani Agosti mwaka 2023.
Dereva wa pikipiki na abiria wake wakizuiwa na polisi kupita, wakati kukishuhudiwa makabiliano baina ya polisi na waandamanai nchini Kenya.Picha: Luis Tato/AFP

Wakati maandamano hayo yakiingia siku ya pili, hali inaelezwa kuwa shwari na hata shule za kutwa zimefunguliwa tena baada ya serikali kuhakiki hali ya usalama wa wanafunzi. Vinara wa upinzani wa Azimio la Umoja bado hawajaonekana hadharani ingawa wanasisitiza maandamano yanaendelea.

Wito wa kukaa kwenye meza ya mazungumzo bado unatolewa kuwarai kiongozi mkuu wa upinzani Raila Odinga na Rais William Ruto kufikia mwafaka. Leo ni siku ya pili ya maandamano ya kuishinikiza serikali na hali jijini Nairobi ni shwari na inarejea kawaida. 

Duru zinaeleza kuwa viongozi wa upinzani wa muungano wa Azimio la Umoja waliokamatwa na polisi bado wanazuiliwa. Mbunge wa Embakasi East Babu Owino anazuiliwa kwenye kituo cha polisi cha Wanguru kilichoko kwenye kaunti ya Kirinyaga kama alivyofahamisha mkewe Frida Ongili. 

Taarifa mpya zinaashiria kuwa mbunge huyo wa Embakasi East amehamishwa kutokea kituo cha polisi cha Wanguru. Kwa sasa mchakato wa viongozi 10 wa Azimio la Umoja kuachiliwa mahakamani umeanza, kwa mujibu wa wakili wao, Danstan Omari.

Soma Zaidi:Maandamano ya upinzani yaendelea kuiandama Kenya 

Maandamano yameligubika taifa la Kenya ya kuishinikiza serikali kupunguza gharama za maisha.
Wito umetolewa kwa rais William Ruto na kiongozi wa upinzani, Raila Odinga kufanya mazungumzo ili kupata amani.Picha: TONY KARUMBA/AFP

Msako ulioanza hapo umemnasa pia kiongozi wa zamani wa kundi la wahalifu la Mungiki, Maina Njenga, usiku wa kuamkia leo. Familia yake sasa inaiomba serikali kufichua aliko baada ya kukamatwa alipovamiwa nyumbani kwake eneo la Matasia la kaunti ya Kajiado.

Wakati huo huo, waziri wa usalama wa taifa kwa ushirikiano na mwenzake wa elimu walitangaza kuwa shule za kutwa zimefunguliwa tena hii leo, ila baadhi ya wanafunzi wameagizwa kurejea nyumbani hapa Nairobi. Wanafunzi wa shule za Kangemi, eneo la barabara ya Juja na Kibera walirejeshwa nyumbani kwa kuhofia usalama wao. Kwenye eneo la kanda ya Ziwa la Nyanza, hali ni shwari kwa ujumla.

Yote hayo yakiendelea, kiongozi wa chama tawala bungeni, Kimani Ichungwah, amemtaka Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Anthony Muheria kuzungumza na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta ili amani idumu nchini Kenya.

Tamko hilo linatolewa baada ya viongozi wa kidini kuwarai viongozi wa serikali na upinzani kukaa kwenye meza ya mazungumzo ya suluhu. Watetezi wa amani wanausisitizia umuhimu wa kurejea kwenye mazungumzo ya suluhu. Hussein Khalid, mkurugenzi wa shirika la Haki Afrika la kutetea haki za binadamu amenukuliwa akisema " Ile nafasi ya viongozi tunayoiona hivi sasa ya viongozi kuweza kukaa chini na kuzungumza ni nafasi ambayo inatakiwa kuchukuliwa na wote  na tuache kujipiga vifua kuonyesha kwamba hatuwezi kuyajadili yale yaliyopo kwenye jamii zetu."

Maandamano hayo ya yamepangwa kuendelea kwa siku ya tatu hapo kesho.

Tizama video: 

Je, maandamano ndio suluhu ya matatizo yanayoizonga nchi?