1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sri Lanka yaadhimisha wiki moja tangu mashambulizi.

28 Aprili 2019

Kiongozi wa Kanisa Katoliki nchini Sri Lanka Kadinali Malcolm Ranjith ameongoza ibada ya faragha Jumapili (28.04.2019) ya kuadhimisha wiki moja tangu mashambulizi dhidi ya makanisa yaliyosababisha vifo vya watu 253.

https://p.dw.com/p/3HZmp
Sri Lanka Colombo Mahnwache vor Anthony's Shrine nach Anschlägen
Picha: Getty Images/AFP/J. Samad

Makanisa nchini humo hata hivyo bado yamefungwa kufuatia hofu ya kiusalama.

Kadinali Ranjith, ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Colombo ametumia ibada hiyo ya misa kulaani vikali mashambulizi hayo ya mambomu wakati wa sherehe za Pasaka, huku akitoa mwito kwa watu kuungana.

Ibada hiyo ilirushwa moja kwa moja na vituo vya televisheni na radio, kufuatia wasiwasi wa mashambulizi zaidi hatua iliyosababisha kuzuiwa kwa ibada za umma makanisani.

Taifa hilo la kisiwa, lenye watu milioni 21 linasalia chini ya ulinzi mkali, ikiwa ni siku saba baada ya washambuliaji wenye itikadi kali kufanya mashambulizi hayo kwenye makanisa na hoteli za kifahari.

Sri Lanka | Soldaten nach Terroranschlag
Ulinzi bado umeimarishwa nchini humo kufuatia hofu kuu ya mashambulizi mengine mapya.Picha: Reuters/D. Liyanawatte

"Hiki ni kipindi ambacho mioyo yetu imejaribiwa na uharibifu mkubwa uliofanywa Jumapili iliyopita makanisani" alisema Kadinali Ranjith alipoongoza ibada hiyo kutoka katika kanisa dogo lililopo kwenye makaazi yake mjini Colombo.

"Tunaomba Mungu awalaze mahala pema peponi wale wote waliopoteza maisha kwenye mashambulizi hayo, tunaomba amani kwenye taifa hili na maelewano baina yetu na kusiwepo kwa migawanyiko", alisema kiongozi huyo huku akilitaja shambulizi hilo kuwa ni "tusi dhidi ya ubinaadamu".

Ibada hiyo maalumu ilihudhuriwa na rais Maithripala Sirisena, waziri mkuu Ranil Wickremesinghe na kiongozi wa upinzani Mahinda Rajapaksa, ambao pia waliwasha mishumaa kuwakumbuka wahanga.