WHO: Mikakati inafaa kuwekwa kupunguza vifo vinavyotokana na ajali za barabarani | Masuala ya Jamii | DW | 07.12.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

WHO: Mikakati inafaa kuwekwa kupunguza vifo vinavyotokana na ajali za barabarani

Ajali za barabarani humuua mtu mmoja kila baada ya sekunde 24, huku vifo milioni 1.35 vinavyosababishwa na ajali za barabarani vikiripotiwa kila mwaka kote duniani. Limesema Shirika la Afya Duniani WHO

Idadi ya ajali za barabarani imeongezeka kwa laki moja katika muda wa miaka mitatu, huku ajali hizo zikitajwa kuwa zinazoongoza katika vifo vya watoto na vijana wa kati ya umri wa miaka mitano na ishirini na tisa, limeeleza Shirika la Afya Duniani WHO kwenye ripoti yake mpya.

Mkuu wa shirika hilo, Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema ajali zinaweza kuzuiwa iwapo mikakati mwafaka itawekwa. Tedros amesema,"Vifo hivi ni malipo yasiyokubalika kwa watembeaji. Hakuna sababu ya hatua kutochukuliwa. Hili ni tatizo lililo na ufumbuzi uliothibitika. Ripoti hii ni mwito kwa serikali na washirika kuchukua hatua madhubuti ya kutekeleza mikakati hii."

Ripoti hiyo ya WHO kuhusu usalama barabarani iliyotathmini data kutoka mwaka 2016, imeonesha kuwa hali inaendelea kuwa mbaya. Katika ripoti yake ya mwisho iliyotathmini data ya mwaka 2013, idadi ya vifo vilivyosababishwa na ajali za barabarani ilikadiriwa kuwa milioni 1.25 kila mwaka.

Lakini licha ya kuongezeka kwa vifo vinavyotokana na ajali za barabarani, viwango vya vifo ikilinganishwa na kuongezeka kwa idadi ya watu na magari duniani imeimarika katika miaka ya karibuni.

WHO imesema juhudi za usalama barabarani katika mataifa yenye kipato cha wastani na cha juu zimesaidia kukabili hali hiyo. Kadhalika imesema hatua hiyo imetokana na sheria bora kuhusu athari kuu ikiwemo mwendo kasi, kuendesha gari ukiwa mlevi na kutofunga mkanda.

Miundombinu salama na kutengwa kwa barabara za waendao kwa miguu pamoja na barabara za baiskeli na viwango bora vya magari pia zimetajwa kuwa sababu zinazochangia kuimarisha hali barabarani. Hata hivyo, licha ya mataifa mengi kuboresha juhudi zake katika kukabili ajali za barabarani, mataifa maskini bado yanasalia nyuma. Kulingana na ripoti hiyo, mataifa yenye pato la chini yamedhihirisha kuwa vifo vinavyotokana na ajali ni mara tatu zaidi kuliko katika mataifa yenye pato kubwa.

Viwango vya vifo hivyo katika mataifa ya Afrika vimetajwa kuwa asilimi 26.6 kwa watu laki moja, ikilinganishwa na Ulaya ambapo ni asilimia 9.3. Wapita njia na waendeshaji baiskeli wanachangia asilimia 26 ya ajali za barabarani, na idadi hiyo ni asilimia 44 katika ukanda wa Afrika.

Waendeshaji pikipiki pamoja na abiria wao wanachangia asilimia 28 ya vifo vya barabarani, lakini idadi hiyo nia ya juu eneo la kusini mashariki mwa Asia ambapo ni asilimia 43.

Mwandishi: Sophia Chinyezi/AFPE

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com