Waziri Ujerumani aipongeza mahakama Uturuki kwa kuwaachia wanaharakati | Matukio ya Kisiasa | DW | 26.10.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Waziri Ujerumani aipongeza mahakama Uturuki kwa kuwaachia wanaharakati

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel ameupongeza uamuzi wa mahakama kuu nchini Uturuki kwa kuwaachia huru wanaharakat wa haki za binadamu pamoja na raia wa Ujerumani,  Peter Steudtner.

Türkei Istanbul Freilassung Peter Steudtner (Reuters/O. Orsal)

Raia wa Ujeruman Peter Steudtner akiwa na wanaharakati wengine wa Shirika la Amnesty mara baada ya kuachiwa huru jana.

.

Sigmar alisema Berlin inafuatilia kuachiwa huru kwa raia mwingine wa Ujerumani ambaye amefungwa katika gereza jingine nchini humo kwa makosa mengine tofauti. 

Mahakama  ya mjini Instabul jana iliamuru wanaharakati  hao wa haki za binadamu wanane, waliokuwa wamewekwa rumande, waachiwe kwa dhamana wakati kesi yao inayohusiana na ugaidi, ikisubiri maamuzi ya mahakama. Watu wawili katika kesi hiyo inayowasisha washukiwa 11 wameachiwa huru, huku mtuhumiwa wa mwisho akishikiliwa katika kizuizi kilichoko katika mji mwingine.

 Watuhumiwa hao, akiwamo Mkurugenzi wa Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Amnesty International nchini Uturuki, Idil Eser, raia wa Ujerumani  Steudtner na Msweden Ali Gharavi, walikamatwa na na polisi wakati walipohudhuria warsha ya mafunzo kuhusu usalama wa mfumo wa kidijitali, mnamo Julai mwaka huu.

 Kesi yao imezidisha wasiwasi kwamba utawala wa Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan unazidi kuwa wa kiimla.

 Washitakiwa wote hao wanatuhumiwa kuandaa  mapinduzi na kusaidia wanaharakati wa Kikurdi  wenye mrengo wa kushoto.

Pia wanashutumiwa kushiriki katika njama ya mhubiri wa kidini aishie nchini Marekani Fethullah Gulen, ambaye serikali ya Uturuki inamtuhumu kuratibu jaribio la mapinduzi ya kijeshi lililoshindwa Julai mwaka jana.

Amnesty yaapa kuendelea na harakati za mapambano 

Deutschland Protest zum Auftakt des Prozesses gegen Steudtner und weitere Menschenrechtler in Berlin (Imago/C. Ditsch)

Wananchi walioshika mabango wakishinikiza kuachiwa huru kwa wanaharakati wa Amnesty International.

Baada tu ya kuachiwa kutoka jela, mjerumani Peter Steudtner alisema, ''Tunawashukuru sana wale wote waliotupa ushirikiano, wa kisheria, wa kidiplomasia na wa kizalendo.''

Kwa upande wake Ali Gharavi alisema hivi sasa wamepata  familia kubwa mpya, na kushukuru mchango wa kila upande katika kuwezesha kuachiwa kwao.

Amnesty International ilikaribisha kuachiwa huru kwa wanaharakati hao na kuapa kuendelea na harakati za kutetea haki za binadamu nchini Uturuki.

 ''Leo, hatimaye, tunasherehekea kuwa marafiki zetu na wenzetu wanarudi kwa wapendwa wao na watalala katika vitanda vyao kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miezi minne,'' amesema  Katibu Mkuu wa Amnesty Salil Shetty.

Sigmar  alisema uamuzi huo wa mahakama umeonyesha kuwa wito wa Ujerumani wa kutolewa kwa hukumu ya haki umesikilizwa..

 Mwenyekiti wa Amnesty, Taner Kilic, ambaye aliswekwa gerezani Juni, kesi yake inasikilizwa katika mahakama tofauti akihusishwa na padri wa Marekani, Fethullah Gulen.

 Kilic anatuhumiwa kuajiriwa na mtandao wa Gulen wa kutumia mfumo wa simu wa meseji za siri.

Gulen mwenyewe ameyakana mashtaka hayo ya kuongoza jaribio la kuipindua nchi.

Uturuki iliwakamata watu 50,000 tangu jaribio la mapinduzi lililoshindwa mwaka jana na kuwafuta kazi serikalini, karibu watumishi 110,000.

 Mwandishi: Florence Majani(AP)

Mhariri: Daniel Gakuba

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com