1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi na China

Abdu Said Mtullya13 Oktoba 2009

Waziri Mkuu wa Urusi Putin aendelea na ziara ya siku tatu nchini China.

https://p.dw.com/p/K56j
Waziri Mkuu wa Urusi Vladimir Putin na mwenyeji wake Wen Jiabao.Picha: AP

Waziri Mkuu wa Urusi Vladmir Putin anaendelea na ziara ya siku tatu nchini China yenye lengo la kuendeleza zaidi uhusiano wa kiuchumi baina ya nchi mbili hizo.

Leo China na Urusi zimetiliana saini makubalino kadhaa , thamani ya dola bilioni 3.5 kabla ya waziri mkuu Putin kukutana na waziri mkuu mwenzake Wen Jiabao wa China.

Ikiwa ni ishara ya dhamira ya kuendeleza zaidi uhusiano katika sekta ya uchumi, waziri mkuu Putin anafuatana na ujumbe wa wajasiramali na wawakilishi kutoka sekta za usafirishaji, miundo mbinu na nishati.

Waziri mkuu wa Urusi Vladmir Putin na mwenyeji wake waziri mkuu wa China Wen Jiabao leo wanatarajiwa kushiriki kwenye sherehe za kuadhimisha miaka 60 ya uhusiano wa kibalozi baina ya nchi zao.

Katika ziara yake nchini China Putin anatarajiwa kutia saini makubaliano juu ya miradi mikubwa ya nishati baina ya nchi yake na China ambayo kwa pamoja itakuwa na thamani ya dola bilioni 5.5

Vyombo vya habari vya serikali vya China vimesema pana uwezekeno wa kufikiwa mapatano juu ya ujenzi wa kinu cha kusindikia mafuta kati ya Urusi na China. Kinu hicho kinatarajiwa kujengwa katika mji wa Tianjin nchini China

Na shirika la habari la Urusi Novosti limearifu kwamba wajumbe wa Urusi na China wamejadili njia za ushirikiano katika sekta ya gesi.

Kutokana na kukabiliwa na athari zilizosababishwa na mgogoro wa uchumi, Urusi sasa inadhamiria kuendeleza biashara kati yake na China katika sekta mbalimbali.

Mwandishi:Hartbrich ,Esthe (Moskau WDR)

Imetafsiriwa na Mtullya Abdu.

Mhariri:Abdul-Rahman