1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu milioni 13 wanahitaji msaada DRC

Saleh Mwanamilongo19 Januari 2018

Mashirika ya WFP, FAO na UNICEF yamesema machafuko kwenye majimbo ya Kassai na Kivu yamesababisha ukosefu wa chakula na kwamba watu milioni 13 wanahitaji msaada kwa dharura

https://p.dw.com/p/2r8aN
Kongo DRK Krankenhaus Hospital Muungan
Picha: DW/Flávio Forner

Mashirika ya kibinadamu ya umoja wa mataifa yanahitaji msaada wa dola bilioni 1,68 kwa ajili ya misaada ya kiutu katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ambako watu zaidi ya milioni 13 wanahitaji msaada wa chakula. Kwenye ripoti yake ya pamoja mjini Kinshasa mashirika hayo yakiwemo WFP, FAO na UNICEF yamesema machafuko kwenye majimbo ya Kassai na Kivu yamesababisha ukosefu wa chakula kwenye maeneo hao na kuelezea uwezekano wa kuweko na baa la njaa ikiwa hakutokuweko na msaada wa haraka.

Mwito huo wa pamoja wa mashirika ya UNICEF, WFP na FAO umefuatia hali ngumu ya kiutu kwenye majimbo ya Kassai mnamo mwaka uliopita. Mashirika hayo yameeleza kuwa watu milioni 13 wanahitaji msaada wa haraka.

Claude Jibidar ambaye ni mwakilishi wa shirika la mpango wa chakula duniani WFP, amesema machafuko kwenye majimbo ya Kassai yalisababisha wakaazi wa majimbo hayo kutolima kwa misimu mitatu mfululizo.

Machafuko katika majimbo ya Kassai yamechangia tatizo la njaa
Machafuko katika majimbo ya Kassai yamechangia tatizo la njaaPicha: Reuters/Kenny Katombe

Kassai: Tishio la kutokea baa la njaa

Claude ameongeza kuwa: "Mwaka uliopita ulikuwa mwaka mgumu sana kwa mamilioni ya raia wa majimbo ya Kassai, kutokana na mfululizo wa machafuko, magonjwa na malisho mabaya. Hali hiyo imesababisha kuweko na tishio la baa la njaa kwenye eneo hilo. Lakini kuna pia wananchi wa maeneo mengine ambao hawana chakula kutokana na machafuko huko mashariki".

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na kuratibu misaada ya kiutu OCHA, limeelezea kwamba mahitaji yameongezeka kufuatia ongezeko la wakimbizi wa ndani nchini DRC. Shirika hilo limeeleza kwamba Kongo ina wakimbizi wa ndani milioni 4.3. Takriban nusu ya wakimbizi hao ni kutoka majimbo ya Kassai na waliyahama makaazi yao mwaka jana.

Mashirika hayo yanaelezea pia kwamba kwenye sekta ya kiafya Kongo ilishuhudia mwaka wa 2017 ugonjwa wa kipindupindu ambao watu 1000 walifariki na watu 55, 000 waliambukizwa.

Wanaohitaji msaada wameongezeka ndani ya miaka miwili

Nusu ya wakimbizi wa ndani wa DRC wanatoka Kassai
Nusu ya wakimbizi wa ndani wa DRC wanatoka KassaiPicha: Getty Images/AFP/P. Moore

Kuna ongezeko la asimilia 30 ya watu wanaohitaji msaada wa chakula ukilinganisha na miaka miwili iliyopita, inaelezea taarifa hiyo ya pamoja ya mashirika ya WFP, FAO na UNICEF. Asilimia 90 ya wakaazi wa majimbo ya Kassai wanaishi kwa kutegemea kilimo, lakini machafuko baina ya jeshi na wapiganaji wa kikabila wa kamwina Nsapu,yaliyodumu miezi 10 yalisababisha watu wengi kuyahama makazi yao.

Taarifa hiyo imeendelea kueleza kuwa "bila msaada wa haraka wa mashirika ya kiutu, hali ya maisha ya maelfu ya wakaazi yatahatarishwa na matumaini ya kuboresha hali hiyo yanaendelea kutoweka. Tunatakiwa kuhakikisha kwamba misaada imewafikia”.

Mashirika hayo yamehitaji dola bilioni 1,6 mnamo kipindi cha mwaka mmoja.

Mwandishi: Saleh Mwanamilongo, DW Kinshasa.

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman