1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 50,000 wauwawa katika vita Sudan Kusini

Admin.WagnerD3 Machi 2016

Takriban watu 50,000 wameuwawa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka miwili Sudan Kusini na kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa hali ya maafa ya kibinadamu inazidi kuwa mbaya kwa kutotekeleza makubaliano ya amani.

https://p.dw.com/p/1I5yP
Watu wanaopotezewa makaazi Sudan Kusini.
Watu wanaopotezewa makaazi Sudan Kusini.Picha: Getty Images/AFP/A. G. Farran

Mkuu wa shughuli za kulinda amani za Umoja wa Mataifa Herve Ladsous amesema maelfu ya watu wameuwawa kiasi kwamba wanashindwa hata kuwahesabu na wengine karibu milioni mbili wamepotezewa makaazi yao katika vita hivyo ambavyo hivi sasa vinaingia mwaka wake wa tatu.

Ladsous amewaambia waandishi wa habari kwamba ingawa makubaliano ya amani yamefikiwa tokea mwezi wa Augusti makundi kuhusika katika mzozo huo yanaburuza miguu katika kutekeleza makubaliano hayo.

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa ameongeza kusema bado hawana serikali ya mpito na hali ya kibinaadamu na kiuchumi ni balaa na inazidi kuwa mbaya.

Kwa mujibu wa afisa wa Umoja wa Mataifa aliyekataa kutajwa jina watu 50,000 wameuwawa katika vita hivyo vya Sudan Kusini na watu milioni 2.2 yumkini hata zaidi wamekuwa wakimbizi au wamepotezewa makaazi yao na kwamba baa la njaa linainyemelea nchi hiyo ambayo inaweza kukumbwa na njaa miezi michache inayokuja.

Mauaji na uharibifu

Umoja wa Mataifa umesema mwezi uliopita kwamba makundi yanayohasimiana Sudan Kusini yanauwa, yanateka nyara, yanawapotezea makaazi raia na kuharibu mali licha ya kauli za usuluhishi zilizotolewa na Rais Salva Kiir na makamo wake wa zamani Riek Machar ambaye amegeuka kuwa hasimu wake.

Watoto katika kambi za kujihifadhi Sudan Kusini.
Watoto katika kambi za kujihifadhi Sudan Kusini.Picha: DW / F. Abreu

Baada ya mazungumzo ya miezi kadhaa na mazungumzo ya kusitishwa kwa mapigano yasiokuwa na tija pande zote mbili zimekubali hapo mwezi wa Januari kushirikiana madaraka katika serikali ya mpito na mwezi uliopita Kiir amemteuwa upya Machar katika wadhifa wake wa zamani.

Afisa wa Umoja wa Mataifa amesema hawakufika popote katika suala la kutekeleza makubaliano ya amani na kwamba wanachokishuhudia ni kuenea kwa matumizi ya nguvu chini ya misingi ya kikabila katika baadhi ya sehemu za Sudan Kusini ambazo hadi sasa zilikuwa hazikuguswa na ghasia hizo.

Kiir na Machar lawamani

Jopo la Umoja wa Mataifa ambalo linafuatilia mzozo wa Sudan Kusini kwa niaba ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limesema hapo mwezi wa Januari kwamba Kiir na Machar bado wana wanadhibiti kikamilifu vikosi vyao na kwa hiyo wanastahiki moja kwa moja kulaumiwa kwa mauaji ya raia.

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini (kushoto) Riek Machar (kulia) katikati ni aliekuwa Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete.
Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini (kushoto) Riek Machar (kulia) katikati ni aliekuwa Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete.Picha: Getty Images/AFP

Wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wanatowa hifadhi kwa takriban watu 200,000 katika vituo sita nchini Sudan Kusini.

Angola imesema wiki iliopita ilipendekeza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liiwekee Sudan Kusini vikwazo vya silaha hatua ambayo pia inashinikizwa na Uingereza lakini Urusi ambayo ina uwezo wa kura ya turufu katika baraza hilo imepinga kwa hoja kwamba itafanya kazi kwa serikali kuliko waasi na haiamini iwapo hatua hiyo inaweza kusaidia.

Wiki iliopita waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amesema Kiir na Machar watakabiliwa na vikwazo binafsi iwapo watashindwa kutekeleza makubaliano ya amani na kuonya kwamba Sudan Kusini iko katika wakati muhimu wa kunusurika kwa taifa hilo.

Mwandishi : Mohamed Dahman /AFP/Reuters

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman