Watu 50 wafa kwa mafuriko Niger | Matukio ya Afrika | DW | 15.09.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

NIGER

Watu 50 wafa kwa mafuriko Niger

Kiasi cha watu 50 wamekufa kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua zilizonyesha kwa miezi mitatu nchini Niger na wengine karibu 120,000 hawana makaazi.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na uratibu wa masuala ya kibinaadamu (OCHA) imesema kuwa mji mkuu wa Niger, Niamey ndiyo umeathirika zaidi pamoja na Dosso, mji ulioko kusini, mji wa Tillaberi ulioko magharibi na maeneo ya katikati mwa nchi na kusini mashariki mwa Maradi na Zinder.

Vifo 21 kati ya 50 vimetokea Niamey, huku watu 47 wakiwa wamajeruhiwa na wengine wapatao 117,600 wakiwa hawana makaazi kutokana na mafuriko hayo.

Umoja wa Mataifa umesema uzalishaji wa chakula pia umeathirika, huku mifugo ipatayo 16,000 ikiwa imekufa na hekta 9,000 za mazao zikiharibiwa.

Nchi hiyo yenye watu milioni 17, ambayo asilimia 75 ya nchi ni jangwa, nchi hiyo inakabiliwa na uhaba wa chakula uliosababishwa na ukame pamoja na mafuriko mabaya.