1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 23 wajeruhiwa katika mashambulizi mbali mbali Ukraine

27 Januari 2026

Vikosi vya Urusi vimewauwa watu wawili na kuwajeruhi takriban 23 wengine wakiwemo watoto wawili na mwanamke mjamzito katika mashambulizi tofauti nchini Ukraine. Haya yamesema leo na maafisa nchini humo.

https://p.dw.com/p/57WEU
Ukraine Kostiantynivka 2025 | shambulizi la Urusi
Shambulizi la Urusi katika mji wa Kostiantynivka, nchini Ukraine, mnamo November 1, 2025.Picha: Jose Colon/Anadolu/picture alliance

Maafisa hao wa Ukraine wamesema makombora na droni za Urusi zimelenga mji wa pili kwa ukubwa nchini Ukraine, Kharkhiv jana jioni na kusababisha kukatizwa kwa nguvu za umeme wakati huu wa msimu wa baridi kali huku watu 23 wakijeruhiwa katika shambulizi la usiku kucha katika mji wa kusini wa Odesa.

Katika ujumbe kwenye mtandao wa Telegram, gavana wa Kharkhiv Oleh Syniehubov, amesema watu wawili walijeruhiwa na shule mbili kuharibiwa katika shambulizi la eneo hilo.

Mwanamume mmoja na mkewe waliuawa katika eneo la Sloviansk katika eneo la mashariki la Donetsk huku picha zilizochapishwa katika mitandao isiyo rasmi ya telegram zikionyesha mji huo wa mashariki wa Donetsk ukiwa gizani.

Gavana wa eneo hilo amesema Urusi ilirusha zaidi ya droni 50 katika eneo hilo na kuharibu majengo kadhaa ya makazi, shule na kanisa.

Katika siku za hivi karibuni, mashambulizi ya droni na makombora ya Urusi yamekatiza nguvu za umeme kwa mamilioni ya raia wa Ukraine kote nchini humo.

Vikosi vya Urusi vyasonga mbele Ukraine

wizara ya ulinzi ya Urusi imesema Gerasimov alikagua hatua zilizopigwa na ujumbe wa kikosi kinachojulikana kama Zapad kinachohusika na vita hasa katika eneo la Kharkiv na mashariki mwa Ukraine.

Urusi 2025 | Valery Gerassimow
Mkuu wa majeshi wa Urusi Valery Gerasimov akiwa katika mkutano na Rais wa Urusi Vladimir Putin mnamo Oktoba 26, 2025 Picha: IMAGO/Kremlin Press Office

Gerasimov amesema kikosi hicho kinaendelea kusonga mbele katika pande zote.

''Tangu mwanzoni mwa Januari, makazi 17 yamekombolewa. Zaidi ya kilomita za mraba 500 za maeneo zimekuwa chini ya udhibiti wetu. Kundi la Vikosi vya Kaskazini linaendesha shughuli za kivita ili kupanua eneo la usalama katika maeneo ya mpaka ya mikoa ya Sumy na Kharkiv. Makazi manne yamekombolewa mwezi uliopita, ikiwa ni pamoja na Semenovka na Staritsa wiki iliyopita.''

Mazungumzo kuhusu Ukraine kufanyika Februari 1

Ziara hii inajiri siku chache baada ya mazungumzo ya pande tatu yaliyosimamiwa na Marekani kufanyika katika Umoja wa Falme za Kiarabu kati ya wapatanishi wa Urusi na Ukraine. Duru nyingine ya mazungumzo inatarajiwa kufanyika Februari 1, hii ikiwa ni kulingana na rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky.

Kuondoka kwa Ukraine Donbas ndio njia ya amani

Katika ujumbe kwenye mtandao wa X,  mjumbe wa rais Putin Kirill Dmitriev amesema kujiondoa kwa Ukraine huko Donbas ndio njia ya kuelekea amani.

Urusi inadhibiti asilimia 90 ya eneo la Donbas na mara kwa mara, Rais Putin amerejelea kuwa ikiwa Ukraine haitaachia maeneo inayoshikilia, basi Urusi itayateka kwa nguvu.