Watu 17 wauawa baada ya maporomoko ya takataka Msumbuji | Matukio ya Afrika | DW | 20.02.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Watu 17 wauawa baada ya maporomoko ya takataka Msumbuji

Mvua kubwa yasababisha vifo vya watu 17 baada ya rundo la takataka kuporomoka mji mkuu wa Msumbiji, Maputo. Mamlaka nchini humo inaamini kuwa watu wengi wamefunikwa kwenye rundo hilo huku shughuli za uokozi zikeindelea.

Maafa hayo yametokea katika mtaa unaokaliwa na watu wengi walio maskini, limesema shirika lahabari la Kireno, Lusa. Urefu wa rundo la takataka hizo ulikuwa sawa na jengo la ghorofa tatu.

Kiasi cha nusu ya nyumba katika eneo hilo ziliharibiwa huku baadhi ya wakaazi wakihama, wakihofia kuporomoka kwa taka nyingine na vifo. Mkuu wa Baraza la Manispaa la mji huo, David Semengo, amethibitisha tukio hilo.

"Tunathibitisha vifo vya watu 17, wakiwemo watu wazima 12 na watoto watano. Tunathibitisha kuwa watu watano wako hospitalini wakiwemo watu wazima watatu na watoto watatu," amesema David Semengo.

Afisa anayeshughulikia majanga ya kitaifa nchini humo, Fatima Belchior, ameliambia shirika la habari la Lusa kuwa mlima huo wa takataka ulipoziromokea familia kadhaa na wengine hadi sasa huenda wamefunikwa na takataka hizo. Mamlaka inajaribu kuokoa watu ambao wamepoteza nyumba zao, ameongeza kusema.

Takataka hizo zimeharibu nyumba za familia tano na makundi ya uokozi yanaendelea na shughuli za kutafuta manusura. Mkaazi mmoja, kwa jina Mario Huo, amesema kuwa anaishi karibu na mlima huo wa takataka kwa kuwa hana mahali pengine pa kuenda. Anaongeza kusema kuwa iwapo serikali ingemwelekeza mahala pengine pa kuishi, angelihama mara moja. 

Müllberg verschüttet Menschen in Mosambik (picture alliance/AP/F. Momade)

Shughuli za uokozi katika jalala la Hulane, Msumbiji

Jalala hiyo ilistahili kufungwa miaka 10 iliyopita

"Watu wengine wawili walipatikana hapo. Hakuna mashine na hakuna usaidizi wowote. Kwa mfano maiti mbili zimeondolewa kwenye taka na hatuna machela za kuwabebea manusura. Ni jambo gumu," amesema Pedro Ndzovo, mkazi mwengine aliyeshuhudia tukio hilo.

Teresa Mongue, mkaazi mwengine wa eneo hilo, anasema kuwa jalala hiyo ilistahili kufungwa miaka 10 iliyopita kwa kuwa imejaa lakini watu wanaendelea kutupa taka humo. Anaongeza kusema kuwa hayo ndio madhara yake sasa.

Jalala la Hulane ni moja kati ya majalala makubwa katika mji mkuu wa Maputo. Watu wengi mara nyingi hutafuta riziki kwenye jalala hilo, kama chakula na vitu vya kuuza.

Mara kwa mara wahudumu wa afya wamekuwa wakielezea wasiwasi wao kuhusu athari za muda mrefu za moshi pamoja na hatari inayozikabili familia zinazoishi karibu na jalala hilo. Maafisa wa manispaa wa mji wa Maputo wamewahi kujadili kuhusu kufunga jalala hilo.

Mvua kubwa zimekuwa zikinyesha katika mji mkuu wa Maputo tangu Jumapili na kusababisha uharibifu wa nyumba, barabara na shule.

Mwandishi: Shisia Wasilwa /AP/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

IJUE DW

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com