1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 11 wameuwawa Kaskazini mwa Ituri

Sylvia Mwehozi
3 Juni 2021

Watu wapatao 11 wameuwawa na kundi moja la wapiganaji huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kufanya idadi jumla ya watu waliopoteza maisha kufikia 70 tangu kuanza kwa wiki hii

https://p.dw.com/p/3uOOL
DR Kongo UN-Soldaten in Djugu-Territorium | Ituri-Provinz nach Unruhen
Picha: AFP/S. Tounsi

Meya wa wilaya ya Mungwalu Jean-Pierre Pikilisende amesema wachimba madini 11 katika eneo lenye utajiri mkubwa wa dhahabu la Djugu, kaskazini mwa jimbo la Ituri waliuwawa na kundi moja la wapiganaji linaloitwa FPIC. Asasi ya KST inayofuatilia masuala ya usalama eneo la mashariki mwa Congo imesema waliouwawa ni 12.

Mikoa ya Ituri na Kivu Kaskazini iliwekwa chini ya mzingirokatika jitihada za serikali za kukabiliana na ongezeko la machafuko kwa kuondoa uongozi wa kiraia na kuweka maafisa wa kijeshi na polisi.

Usiku wa kuamkia Jumapili watu 53 waliuwawa katika vijiji viwili vya Tshabi na Boga mkoani Ituri, ikiwa ni mauaji makubwa kutokea ndani ya siku moja katika siku za hivi karibuni. Mwandishi wa habari wa AFP alisema wanamgambo hao waliilenga kambi ya watu waliokosa makaazi na karibu mabanda 84 yaliteketezwa pamoja na maduka 8 huko karibu na Boga. Watu wengine watano waliuwawa mapema siku ya Jumanne na mzee mmoja alichinjwa Jumatano katika kijiji cha Bulire karibu na Boga.

DR Kongo 2003 | Milizen
Wanamgambo katika eneo la mashariki mwa CongoPicha: Stephen Morrison/dpa/picture alliance

Asasi ya KST inakadiria kwamba karibu raia 1,228 wameuwawa katika eneo la Beni pekee huko Kivu Kusini tangu mwaka 2019 wakati jeshi la Congo lilipoanzisha operesheni dhidi ya waasi na kusababisha kundi la ADF kugawika katika makundi madogo ya wapiganaji.

Naye mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel, Denis Mukwege, amewahimiza wanasiasa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kujihusisha na mapambano dhidi ya udhalilishaji wa ngono na mauaji ya raia mashariki mwa nchi hiyo.

Mukwege alikuwa amealikwa na spika wa bunge la mkoa wa Kivu Kusini kuwahutubia wabunge kuhusu suala la unyanyasaji kingono na utumiaji wa ubakaji kama silaha ya vita nchini Congo.

"Hii ni ishara ya ufahamu wa wawakilishi wa watu waliochaguliwa kuwa ushiriki wao mzuri na endelevu katika vita dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia, katika vita dhidi ya kutoadhibiwa na katika ujenzi wa amani ya kudumu katika mkoa wetu inaweza kuleta tofauti."

Matamshi ya Mukwege yamekuja siku moja baada ya serikali ya Congo mjini Kinshasa kuapa kuharakisha kampeni ya usalama eneo la mashariki, ambako mamia ya watu wameuwawa na makundi ya waasi tangu mwanzoni mwa mwaka huu.