1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 100 wauawa katika mashambulizi ya kikabila Mali

11 Juni 2019

Karibu watu 100 wameuawa katika shambulizi kali la usiku kucha katika kijiji kimoja cha katikati mwa Mali, ikiwa ni tukio la karibuni la umwagaji damu kulikumba eneo hilo tete

https://p.dw.com/p/3K9mB
Mali | Kuhherde in Segou
Picha: Imago Images/Le Pictorium/N. Remene

Hakujawa na taarifa yoyote ya anayedai kuhusika lakini mauaji hayo ya kinyama, yaliyokilenga kijiji cha watu wa jamii ya Dogon, yalikuwa na dalili za mashambulizi ya kikabila ya kulipiza kisasi ambayo yamesababisha vifo vya mamia ya watu. Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani ya Mali Amadou Sangho amesema watu wengine 19 hawajulikani waliko baada ya kijiji hicho kuvamiwa majira ya saa tisa usiku.

Mashambulizi hayo yametokea ikiwa ni miezi mitatu tu baada ya karibu watu 160 wa jamii ya Fulani kuchinjwa na kundi lililotambuliwa kuwa la Dogon. Rais wa Mali Ibrahim Boubacar Keita ameiambia televisheni ya taifa akiwa Uswisi kuwa nchi yake haiwezi kuongozwa na mzunguko wa mashambulizi ya kulipiza kisasi. 

Keita amekatiza ziara yake ya kiserikali kutokana na mauaji hayo. Maafisa wa wilaya ya Koundou, ambako kijiji cha Sobane-Kou kilishambuliwa wamesema watu 95 waliuawa, miili yao ikachomwa na wengine bado hawajulikani waliko

Kiongozi wa kundi la wanamgambo wa Dogon amepinga kuhusika kwa wapiganaji wake kwenye tukio la mwenzi Machi ambalo watu 157 walikufa lakini viongozi wa jamii ya Peuhl waliahidi kutekeleza mauaji ya aina hiyo kulipa kisasi.

Uhasama baina ya makabila umeongezeka miaka ya karibuni katika eneo la kati ya Mali kutokana na uwepo wa makundi ya itikadi kali yalihamia kutoka kaskazini mwa nchi hiyo.