Watoto wanajeshi walioporwa utoto wao
Wana miaka saba au nane tu, lakini hulishwa madawa ya kulevya, na kulaazimishwa kuuwa watu kwa kutumia silaha: Wanajeshi watoto hupitia hali ya kutisha. Wachache wanafanikiwa kurejea katika maisha ya kawaida.
Huburutwa kwenye migogoro
Nyumba zilizopigwa kwa mabomu, wanafamilia waliouwawa au marafiki walliojeruhiwa: Vita huwaathiri zaidi watoto, kama ilivyo hapa katika mji wa Syria wa Aleppo. Watoto wengi huburuzwa katika mgogoro na wanalaazimika kupigana, ili kulinda makaazi yao na kuweza kujinusuru wenyewe.
Katika jina la ugaidi
Kundi la kigaidi la Dola ya Kiislamu IS hutumia vurugu hata dhidi ya watoto: Kulingana na Umoja wa Mataifa, IS iliwatumia watoto kama waripuaji wa kujitoa muhanga au ngao za kibinaadamu. Baadhi wanalaazimishwa hata kuuwa watu. Licha ya vitendo vya kinyama vya IS, kundi hilo bado linawavutia vijana.
Si tu katika uwanja wa vita
Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF, watoto wadogo huandikishwa jeshini na makundi ya waasi na wanamgambo wanaoiunga serikali katika migogoro - ikiwa ni pamoja na wavulana na wasichana. Mayatima ama huuzwa au kutenganishwa na familia zao, kisha wanalaazimishwa kushiriki mapigano, kushughulikia ugavi au hata kutumikishwa kingono.
Watoto 250.000 wanashiriki vita
Sudan, Sudan Kusini, Somalia, Chad - hayo ndiyo baadhi ya mataifa ambako watoto wamelazimishwa kupigana vita katika miaka iliyopita. Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa watoto 250,000 wanatumikishwa na jeshi au waasi katika mapambano ya kivita. Ripoti ya Umoja wa Mataifa inaorodhesha pande 52 za kivita katika mataifa 23 ambazo zinawatumikisha vibaya watoto.
Kupitia madawa ya kulevya
Kwa bahati mbaya matumizi ya watoto yana faida nyingi kwa makundi ya silaha, alisema Ninja Charbonneau wa UNICEF katika mahojiano na DW: "Watoto ni wapiganaji wasio ghali na ambao ni wepesi wa kudanganya. Mara nyingi hulishwa madawa ya kulevya na kupewa propaganda na kuonyeshwa filamu za ukatili. Wanaishi katika hofu ya kuuawa ikiwa watakaidi amri za wakubwa wao.
Msaada kupitia wanajeshi wa kulinda amani wa UN
Wakati mwingine watoto hufanikiwa kutoroka au kukombolewa na wanajeshi wa serikali. Wanajeshi hawa watoto wanakabidhi silaha zao kwa vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa, na kisha hupatiwa mgao wa chakula na dawa. Watoto wanajeshi wanakabiliwa hasa na tatizo la utapiamlo, vidonda vilivyoambukizwa, magonjwa ya zinaa na athari za madawa ya kulevya na matatizo ya akili.
Kurejea katika maisha ya kawaida
Watoto hukabiliwa na ugumu katika kuanza maisha upya na kusahau waliyopitia. Miili yao na roho zao zimejaa makovu. Hivyo ni muhimu kwao kushirikishwa tena katika jamii. Katika makambi, watoto hupelekwa shuleni hadi familia zao zinapowafuata. Lakini hili linachukuwa muda na linakuwa gumu pale migogoro ya kivita inapokuwa inaendelea.
Kukabiliana na kumbukumbu
Moja aliefanikiwa kutoka ni China Keitetsi. Kama mwandishi, anakabiliana na uzoefu wake wa kikatili kama mwanajeshi mtoto wa zamani nchini Uganda katika kitabu chake "Machozi kati ya mbingu na Dunia". Anasimulia juu ya miaka ya kwanza baada ya kukimbilia nchini Denmark, na kujaribu kusahau ukatili wa vita na kujifunza kuishi maisha yasiyo na wasiwasi.
Furaha kamili
Pia Emmanuel Jal alikuwa mwanajeshi mtoto. Hii leo ni nyota wa kimataifa wa muziki wa Hip Hop. Lakini pia hawezi kusahau uzoefu mbaya wa vita. Mashairi yake yanahusu vita nchini Sudan. " Kupitia mashairi ya nyimbo, mtu anaweza kuwasabishia watu kuuawana au kusameheana," anasema mwanaharakati huyo wa amani kwa sasa.
Siku ya kuwakumbuka watoto wanaotumikishwa vitani
Protokali ya hiari kwa Mkataba wa kimataifa kuhusu haki ya mtoto juu ya ushirikishwaji watoto katika migogoro ya kivita imeridhiwa na mataifa 150. Protokali hiyo ilianza kutekelezwa mnamo Februari 12, 2002. Tangu wakati huo dunia imekuwa ikiadhimisha siku ya kuwakumbuka watoto wanaotumikishwa vitani. Siku hiyo inaadhimishwa kila 12 mwezi wa Februari kukumbuka hatma ya watoto hao.
Ni lini mtoto anakuwa mtoto?
Kulingana na Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu watoto wa mwaka 1989, kila mshiriki wa vita alie chini ya miaka 15 ni mwanajeshi mtoto. Mwaka 2002 umri wa kuandishwa jeshini ulipandishwa hadi miaka 18. Usaili wa kujitolea kwa walio zaidi ya miaka 14 ni halali chini ya sheria za kimataifa. Lakini kwa mashirika ya haki za binaadamu, wapiganaji wote walio chini ya miaka 18 ni wanajeshi watoto.