Watawala wa kijeshi Mali waahirisha mkutano wa kwanza wa kurejesha madaraka kwa raia | Matukio ya Afrika | DW | 30.08.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Mali na harakati za utawala wa raia

Watawala wa kijeshi Mali waahirisha mkutano wa kwanza wa kurejesha madaraka kwa raia

Watawala wa kijeshi nchini Mali wameahirisha mkutano wao wa kwanza uliohusu mpango wa kurejesha madaraka kwa raia baada ya kuongezeka kwa mvutano miongoni mwa viongozi wakuu ambao walisababisha mapinduzi ya Agosti 18.

Wanajeshi waliyaalika makundi ya asasi za kiraia, vyama vya siasa na waasi wa zamani kwa lengo la kufanikisha mashauriano. Lakini taarifa ya watawala hao wa kijeshi ilieleza kwamba mkutano umeahirishwa katika dakika za mwisho hapo jana hadi utakapotajwa tena kutokana na kile walichosema "sababu za kimaandalizi".

Mali Bamako Verhandlungen zwischen ECOWAS und Militärführern (Reuters/M. Keita)

Wajumbe wa ECOWAS wakiwa mjini Bamako

Kutoshiriki kwa kundi lililokuwa linampinga Ibrahim Boubacar Keita

Kundi la muungano wa waandamanaji ambalo lilikuwa likifanya maandamano dhidi ya rais wa zamani Ibrahim Boubacar Keita, linalojulikana kama "June 5 Movement" halikualikwa kushiriki mkutano huo. Kundi hilo linataka utawala wa kijeshi kuwajibika katika kufanikisha utawala wa kiraia kama ulivyoahidi, pamoja na kutoainishwa muda.

Tahirou Bah kutoka katika kundi liitwalo Espoir Malikoura, likiwa moja ya nguzo za harakati ya Juni 5, zilizomtoa madarakani Keita, alisema wanasikitika kwa kuanza kwa machungu ya utawala huo wa kijeshi ambao ulizusha matumani mapya kwa umma wa raia wa Mali kwa hivi sasa kwa kuyatenga makundi yenye uwakilishi wa raia.

Mapinduzi yaliyoitikisa Afrika Magharibi na ulimwengu kwa ujumla

Mapinduzi ya Mali yameyatikisa sana mataifa jirani katika eneo la Afrika Magharibi na mshirika wake Ufaransa, jambo ambalo limeongeza wasiwasi zaidi wa hali ya usalama, kwa taifa hilo amablo lipo katika kujikwamua na tatizo la uwepo wa makundi ya wenye itikadi kali, mapigano ya kikabila na shida ya uchumi.

Imam mwenye ushawishi mkubwa nchini Mali, Mahmoud Dicko, ambae alikuwa na ushiriki muhimu katika maandamano ya umma ambayo yalimuondoa rais Keita amesema utawala wa kijeshi hauna mamlaka kamili ya kuiendesha Mali kwa niaba ya wananchi. Watu wamepoteza maisha yao katika kulipiganmia taifa hilo kwa hivyo jeshi lazima litende kwa vitendo ahadi yake ya kuliachia taifa kwa mamlaka ya umma.

Soma zaidi:Viongozi wa Afrika Magharibi wataka jeshi liachie madaraka Mali

Ibrahim Boubacar Keita mwenye umri wa miaka 75 alichaguliwa kidemokrasia kwa mara ya kwanza mwaka 2013, na kutazamawa kama mtu ambae angefanikisha umoja na mshikamano wa nchi na kurejeshwa tena katika muhula wa pili wa miaka mitano 2018, kabla ya kuondolea kwake madarakani kwa mtutu wa bunduki Agosti 18, 2020.

Chanzo: AFP