1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiUganda

Wataalamu wa afya watahadharisha juu ya mzozo wa lishe

1 Juni 2023

Wataalamu wa afya ya lishe Mashariki mwa Afrika wanaonya kuwa mzozo wa lishe ni hali halisi katika mataifa 10 eneo hilo na unahitaji kutafutiwa ufumbuzi wa dharura.

https://p.dw.com/p/4S1k6
Picha hii inamuonyesha raia wa Sudan Kusini akiwa tayari kabisa kupata mlo wake. Mzozo nchini humo unaibua kitisho cha njaa na ukosefu wa usalama wa chakula.
Jamii kubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki inakabiliwa na upungufu wa chakula kutokana na sabab mbalimbali kama ukame.Picha: Elna Schutz/DW

Wajumbe kutoka mataifa hayo wanakutana Uganda kubadilishana maarifa na uzoefu kuhusu jinsi ya kukabiliana na kiwango cha juu cha utapiamlo, njaa na pia magonjwa yanayohusiana na lishe isiyofaa.

Mzozo wa lishe unaelezewa na Shirika la Afya duniani WHO  pamoja na mamlaka ya maendeleo ya serikali za pembe ya Afrika IGAD kutokana na mabadiliko ya tabianchi, ukosefu wa usalama na bei ya juu ya vyakula.

Mzozo huu unatajwa kutishia ongezeko la utapia mlo katika mataifa ya pembe ya Afrika, bonde la mto Nile, pamoja na kanda ya maziwa makuu na hasa kwa watoto walio chini ya miaka mitano, mama zao pamoja na wakongwe wasioweza kujitafutia riziki ya kila siku. Fatuma Adan ni mratibu wa shirika la IGAD kuhusiana na masuala ya afya na lishe."Iko shida, na hiyo shida inatokana na ama mvua kuwa nyingi, au kidogo ama mvua kutonyesha kabisa. Haya yote yanasababisha kuwepo kwa upungufu wa chakula."   

Kulingana na takwimu ambazo zimekusanywa na mashirika mbalimbali ikiwemo lile la mpango wa chakula duniani WFP, viwango vya utapiamlo na njaa viko juu katika mataifa ya Ethiopia, Kenya na Somalia. Hadi watu milioni kumi katika nchi hizo wanahitaji misaada ya lishe.

Watoto wa chini ya miaka mitano ni waathirika zaidi wa ukosefu wa lishe bora kama mtoto huyu wa miaka miwili Aden Salaad. Mtoto huyu alikuwa anapata huduma ya lishe iliyotolewa na madaktari wasio na mipaka nchini Somalia, 2021.
Janga la njaa na upungufu wa chakula limekuwa likiinyemelea Somalia kutokana na kukosekana kwa mvua kwa muda mrefu. Picha: AP

Ijapokuwa hali ya lishe ni afadhali katika mataifa mengine kwa ulinganisho, tatizo kubwa ni bei ya chakula ambayo imesababishwa na misukosuko ya kiuchumi duniani kutokana na vita na pia hali ya jamii nyingi kuendelea kutegemea tu misimu ya mvua.

Hali hii imelezewa kushuhudiwa katika mataifa ya Rwanda, Burundi, Uganda, Tanzania na mataifa jirani kusini mwa Afrika ikiwemo Msumbiji. Wataalamu wanatoa mfano wa bei ya mazao ya nafaka na mengine kama vile maharage kuwa ya juu. Doreen Marandu, afisa mipango katika shirika la ECSA lenye makao yake makuu Arusha Tanzania amesema "Sisi kama wataalamu wa lishe tunawashauri watu wetu kula vyakula vyenye lishe na kuepuka vyakula vyenye sukari na mafuta mengi. Lakini pia tunasisitiza tujaribu kurudi kwenye vyakula vya asili."  

Lakini si kwamba mzozo wa lishe unaathiri tu familia masikini. Hata zile zilizo na uwezo zinakumbwa na magonjwa yatokanayo na unene na yale yasiyo ya kuambukizwa. Hii ni kutokana na wengi kutojua lishe bora.

Mtandao huu wa wataalamu wa kufuatilia hali ya lishe Mashariki mwa Afrika ujulikanao kama LENNS umendelea kujitokeza na mikakati na takwimu mbalimbali baada ya kuendesha warsha zingine nchini Kenya na Tanzania hapo awali. Wanatoa mwito kwa serikali anuwai kuzingitia na kutekeleza mapendekezo wanayowasilisha ili kukabiliana na mzozo huo wa lishe.