Washington. Vimbunga zaidi huenda vikatokea.
26 Septemba 2005Idara ya hali ya hewa nchini Marekani imetoa tahadhari kuwa kuna uwezekano wa kutokea vimbunga zaidi pamoja na mafuriko baada ya kimbunga Rita ambacho kilishambulia majimbo ya Texas na Luoisiana.
Kimbunga Rita kiliambatana na mvua kubwa na upepo unaokwenda kwa kasi ya kilometa 200 kwa saa wakati kilipofika katika ardhi ya Marekani siku ya Jumamosi, na kusababisha uharibifu mkubwa .
Hata hivyo , maafisa wamesema kuwa uharibifu haukuwa mkubwa sana kama ilivyotarajiwa.
Rais wa Marekani George W. Bush ametoa wito kwa kiasi cha watu milioni tatu waliokimbia kutoka katika eneo hilo la kimbunga kutorejea kwa haraka majumbani mwao.
Bush pia amesema kuwa baraza la Congress nchini humo linapaswa kufikiria kulipa jeshi nafasi ya mbele katika uratibu wa kuyashughulikia masuala ya maafa yanayosababishwa na hali ya hewa. Ametoa maelezo hayo baada ya kukutana na maafisa wa vikundi vya uokozi katika eneo la San Antonio.