Washindi wa pili Afrika; Wapinzani wa Maisha?
Sio tu viongozi wa serikali, lakini pia viongozi wa upinzani katika mataifa mengi ya Afrika wamekuwapo kwenye nafasi zao kwa miongo kadhaa. Hapa tunawaletea viongozi wa upinzani waliokaa muda mrefu.
Zimbabwe: Morgan Tsvangirai vs Mugabe
Mchimba madini wa zamani amekuwa ishara ya upinzani dhidi ya rais wa muda mrefu Robert Mugabe. Alianzisha chama cha upinzani cha "Movement for Democratic Change" na amekuwa akikamatwa, kudhalilishwa na kuvunjwa fuvu la kichwa. Kulikuwa na jaribio la kutaka kumrusha kutoka ghorofa ya 10. Baada ya uchaguzi uliogubikwa na utata mwaka 2008, Tsvangirai alisaini makubaliano ya kushirkiana na Mugabe.
Mpiganaji wa msituni wa Msumbiji
Ni mmoja ya wapinzani wa muda mrefu barani Afrika. Afonso Dhlakama alichukua uongozi wa taasisi iliyokuwa ya wapiganaji wa msituni RENAMO mwaka 1979 wakati wa vita nchini Msumbiji. Baadaye kundi hilo liligeuka kuwa chama cha siasa. Hata hivyo, Dhlakama bado anajulikana kwa sauti yake na amesema anaweza kuchukua tena silaha. Mpaka sasa amejaribu kuwania urais kwa mara tano bila mafanikio.
Waziri wa zamani DRC aliyegeuka mkosoaji wa utawala
Etienne Tshisekedi amewahi kuwa waziri wa sheria kabla ya kuhitimu Chuo Kikuu. Baadaye alikuwa raia wa kwanza wa Kongo kupata shahada ya uzamivu ya sheria. Amefanya kazi wakati wa Rais Mobutu Sese Seko lakini baadae akaanza kuikosoa serikali ya DRC na kukamatwa mara kadhaa. Amekuwa kiongozi mkuu wa upinzani nchini humo tangu mwaka 2001. Mwaka 2011 alishindwa na rais wa sasa Joseph Kabila.
Kenya: Siasa kama mambo ya familia
Raila Odinga, mtoto wa makamu wa kwanza wa rais wa Kenya, bado ana matumaini ya kuwa rais siku moja. Pamoja na baba yake, kaka yake, aliwahi kuwa mbunge wa bunge la Kenya, ingawa si miongoni mwa wanachama watiifu ndani ya chama. Ameshahama chama chake mara nne mpaka sasa. Baada ya kushindwa mara tatu, mwaka 2013 Raila Odinga alikwenda mahakamani kupinga matokeo na kuangushwa tena.
Adui namba moja wa umma nchini Uganda
Kiiza Besigye aliwahi kuwa mshirika wa karibu wa Rais Yoweri Museveni wa Uganda na daktari wake binafsi. Lakini kwa sasa ni adui mkubwa wa Ikulu tangu ijulikane wazi kuwa naye anawania kuingia madarakani. Mara kadhaa ametuhumiwa kwa makosa mbalimbali, amekamatwa, kupigwa vibaya. Ameshitakiwa kwa kosa la uhaini bada ya kuandaa maandamano ya kupinga kuchaguliwa tena kwa Rais Museveni mwaka 2016.
Sura muhimu za upinzani nchini Chad
Saleh Kebzabo (kushoto) na Ngarlejy Yorangar wanawakilisha pande mbili tofauti za kisiasa, lakini wote wamekuwa wakipigania mabadiliko ya kisiasa kwa muda mrefu. Hata hivyo, muungano wao ulidhoofika kabla ya uchaguzi mwaka huu kwa sababu walishindwa kukubaliana namna ya kusaidiana. Wakati huo rais Idriss Deby ambaye amekuwepo madarakni kwa miaka 26 sasa alichaguliwa tena kwa kipindi cha tano.
Seif Sharif Hamad na siasa za Zanzibar
Seif Sharif Hamad kiongozi wa upinzani Zanzibar. Ni katibu mkuu wa chama cha CUF. Amegombea mara tano na kushindwa katika matokeo yaliyo na utata. 2001 baada ya mauaji ya wafuasi wa CUF, serikali iliketi meza moja na Seif hadi 2010 ilipozaliwa serikali ya Umoja wa Kitaifa na kuwa makamu wa kwanza wa rais. Katika Uchaguzi wa 2015, Seif alijitangazia ushindi kabla ya uchaguzi huo kufutwa.
Mara ya tatu na ya bahati kwa Akufo-Addo?
Baba wa Nana Akufo-Addo alikuwa rais wa Ghana miaka ya 70, lakini mpaka sasa hajaweza kuvaa viatu vyake. Watu wengi nchini humo wanamdhihaki kwa nia yake ya kutaka madaraka. Hawawezi kumfananisha na mtu wa daraja la juu. Mwezi Novemba atajaribu kwa kipindi cha tatu, na hiyo inaweza kuwa mara yake ya mwisho kwa kuwa chama chake hakina umoja tena.