1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapinzani wajitokeza kumng'oa madarakani Sassou Nguesso

14 Februari 2026

Wagombea sita wa upinzani nchini Kongo Brazzaville, wamejiandikisha kugombea kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa Machi 15, katika harakati za kumngoa madarakani rais wa sasa Denis Sassou Nguesso.

https://p.dw.com/p/58lqu
BG Rangliste der Langzeitherrscher | Kongo Präsident Denis Sassou Nguesso
Rais wa Kongo Brazzaville Denis Sassou Nguesso Picha: Russian Foreign Ministry Press Service/TASS/dpa/picture alliance

Uongozi wa zaidi ya miongo minne wa Sassou Nguesso katika nchi hiyo iliyo tajiri kwa mafuta, unamuweka kuwa moja ya viongozi waliosalia kwa muda mrefu zaidi madarakani, baada ya Paul Biya wa Cameroon, ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1982 na mwenzao wa  Equatorial Guinea Teodoro Obiang Nguema Mbasogo, aliyechukua madaraka kupitia mapinduzi mwaka 1979.

Nguesso aliye na miaka 82 ana umri wa zaidi ya mara mbili ya mpinzani wake kijana mdogo Destin Gavet wa chama cha Republican Movement (MR).

Mwanasheria Vivien Manangou wa chama cha Alliance na Dave Mafoula, waliowahi kugombea urais mwaka 2021 wanatarajia pia kuingia katika kinyanganyiro cha mwaka huu. Orodha hiyo pia inawajumuisha Joseph Kignoumbi Kia Mboungou, aliyeshindana na rais Sassou Nguesso kwa mara ya kwanza mwaka 2002 na Anguios Nganguia Engambe, anayewania kiti hicho kwa mara ya nne sasa.

Mahakama ya katiba inatakiwa kuthibitisha maombi ya wagombea hao kabla majina yao kuchapishwa kwenye orodha ya mwisho ya wagombea. Kampeni za uchaguzi zinatarajiwa kuanza Februari 28 hadi Machi 13.