1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanyarwanda wataka Kabuga ashtakiwe nyumbani

Deo Kaji Makomba
4 Juni 2020

Wanyarwanda wengi walisubiri kwa hamu kukamatawa kwa Felicien Kabuga ambaye alifanikiwa kuukwepa mkono wa sheria mara kadhaa katika kipindi cha miaka 26 kabla ya kunaswa mjini Paris mwezi Mei.

https://p.dw.com/p/3dFMi
Mnyarwanda aliyeponea mauaji ya halaiki akifuatilia kukamatwa kwa Kabuga
Picha: Reuters/J. Bizimana

Wengi walitaka Kabuga ashtakiwe nchini Rwanda, lakini mahakama ya Ufaransa imeamua akabidhiwe kwa Umoja wa Mataifa, hatua ambayo pia manusura wa mauaji ya kimbari ya 1994 wameikaribisha. Wawakilishi wa manusura wa mauaji ya kimbari wanasema wameridhishwa na hukumu ya mahakama ya mjini Paris kwamba Felicien Kabuga anapaswa kuhamishiwa katika mahakama ya kimataifa. Rais wa kundi la manusura wa mauaji hayo Etienne Nsanzimana, ambaye anasema sehemu ya familia yake ilifyekwa katika mauaji hayo, aliliambia shirika la habari la Ujerumani dpa, hapo jana, kwamba "sote tunamtaka awajibishwe."

Mmoja wa manusura wa mauaji hayo Charles Ngarambe, amesema kuwa, walikuwa na wasiwasi kwamba Bwana Felician Kabuga angekufa kabla ya haki haijapatikana. Kwa sasa kuna unafuu kwamba Bwana Kabuga anakwenda kusimama kizimbani kujibu mashitaka yanayomkabili.

Bwana Ngarambe alikuwa ni mwalimu katika shule moja huko Mukarange kaskazini mwa mkoa wa Byumba, alikokuwa akiishi Bwana Kabuga. Alifanikiwa kutoroka nchini Rwanda siku chache tu kabla ya mauaji ya kimbari yaliyotokea mnamo mwaka 1994, lakini alipoteza ndugu zake tisa katika familia yake.

Kabuga alikuwa akiishi Ufaransa

Kabuga alikuwa akitumia vitambulisho feki
Kabuga alikuwa akitumia vitambulisho fekiPicha: Getty Images/AFP/S. Wohlfahrt

Mahakama imeruhusu Kabuga akabidhiwe katika mahakama maalumu ya kimataifa ya makosa ya uhalifu wa mauaji ya kimbari, IRMCT yenye makao yake mjini Arusha, Tanzania, ambayo imekuwa ikishughulikia kesi za mauaji hayo nchini Rwanda.

Akielezwa kama mtu anaetafutwa zaidi barani Afrika, Kabuga alikamatwa Mei 16 nyumbani kwake nje ya mji wa Paris, ambako alikuwa akiishi kwa jina la uongo. Mawakili wake wamehoji kuwa mtuhumiwa huyo mwenye umri wa miaka 84 anapaswa kuruhusiwa kubakia nchini Ufaransa kwa sababu ya umri wake mkubwa, hali dhaifu ya afya na madai ya ukosefu wa usawa ulioonyeshwa na mahakama za kimataifa.

Jaji mjini The Hague, Uholanzi alihukumu mwezi uliyopita kwamba Kabuga anapaswa kushtakiwa mjini Arusha, chini ya mfumo wa wa mahakama ya Umoja wa mataifa MICT.

Alhamis iliyopita mshukiwa mwingiene wa mauaji ya kimbari, Ladislaus Ntagazwa, alihukumiwa kifungo cha maisha jela na mahakama ya Rwanda. Alikamatwa nchini Congo mnamo mwaka 2015 na kisha kurudishwa nchini Rwanda ambako kesi yake ilisikilizwa.

Kabuga ashukiwa kufadhili mauaji ya kimbari 1994

Watu wapatao milioni moja waliuliwa katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda
Watu wapatao milioni moja waliuliwa katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini RwandaPicha: Getty Images/AFP/Y. Chiba

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa mauaji ya kimbari ya Rwanda, ICTR, ni mahakama maalumu iliyoanzishwa jijini Arusha nchini Tanzania na kuwatia hatiani angalau wahalifu 60 ambao walianzisha na kuchochea mauaji hayo ya kimbari. Kesi zilizobakia ziliachwa kwa mahakama ya IRMCT ambayo ni mrithi wa mahakama ya ICTR.

Jean Damcene Bizimana, katibu mtendaji wa CNLG, bodi ya Wanyarwanda, ilioanzishwa kupigana na itikadi ya mauaji ya kimbari, alisema kwamba ingawa Kabuga hajachukua bunduki, lakini alitumia pesa zake kuratibu mauaji ya kimbari.

Kulingana na barua ya mwendesha mashtaka mkuu wa Paris alieshughulikia kesi hiyo, amesema kuwa Kabuga alikuwa akiishi bila kukamatwa nchini Ujerumani, Ubelgiji, Kongo Kinshasa, Kenya na Uswizi na alikuwa akiishi kwa kutumia kitambulisho cha bandia katika kitongoji cha Paris wakati wa kukamatwa kwake.

Kabuga anatuhumiwa kufadhili mauaji hayo ya kimbali na kuagiza idadi kubwa ya mapanga kutoka China ambayo wanamgambo wa Interahamwe walitumia kuwachinja waathirika wa mauaji hayo.

Mfanyabiashara tajiri wa Kihutu, na rafiki wa rais wa zamani wa Rwanda Juvenal Habyarimana, Kabuga alishtakiwa mnamo 1997 kwa makosa saba, kujihusisha katika mauaji ya kimbari, uhamasishaji wa moja kwa moja na wa umma kufanya mauaji ya kimbari, jaribio la kufanya mauaji ya kimbari, njama ya kufanya mauaji ya kimbari, mateso na kuangamiza kuhusiana na mauaji ya Watutsi na makabila ya wastani ya Wahutu nchini Rwanda.

Mwandishi: Deo Kaji Makomba

Mhariri: Iddi Ssessanga