Wanasiasa Guinea Bissau waachiwa huru | Matukio ya Kisiasa | DW | 28.04.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Wanasiasa Guinea Bissau waachiwa huru

Wanajeshi waliofanya mapinduzi nchini Guinea Bissau wamewaachia huru viongozi wa serikali iliyopinduliwa, na kukubali kupelekwa nchini humo kikosi cha Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi, ECOWAS.

Carlos Gomes Junior

Carlos Gomes Junior

Aliyekuwa waziri mkuu na pia akiongoza duru ya kwanza ya uchaguzi, Carlos Gomes Junior (pichani hapo juu), na Raimundo Pereira ambaye alikuwa kaimu rais, waliachiwa Ijumaa jioni, na kusafiri kwa ndege kwenda mjini Abidjan, Cote d'Ivoire. Kuachiwa kwao kulifuatia ziara ya viongozi wa kijeshi kutoka jumuiya ya ECOWAS mjini Bissau.

Alhamisi, ECOWAS ilikuwa imesema itapeleka kikosi chenye wanajeshi zaidi ya 600 nchini Guinea Bissau kusaidia kurejesha utawala wa kiraia, na kutishia kuwawekea vikwazo wanajeshi waliofanya mapinduzi ikiwa watauzuia mchakato huo.

Uchaguzi uliokatizwa

Wanajeshi waliofanya mapinduzi walisema walizima mpango wa kuliangamiza jeshi la Guinea Bissau

Wanajeshi waliofanya mapinduzi walisema walizima mpango wa kuliangamiza jeshi la Guinea Bissau

Mapinduzi ya terehe 12 Aprili yalifanyika wakati taifa hilo la Afrika Magharibi likijiandaa kufanya duru ya pili ya uchaguzi. Guinea Bissau imepita katika misukosuko mingi kisiasa tangu ilipojipatia uhuru kutoka kwa wakoloni wa kireno mwaka 1974.

Msemaji wa kundi la wanajeshi waliofanya mapinduzi, Luteni Kanali Daha Bana na Walna alithibitisha kuachiwa kwa Gomes Junior na Pereira, na kusema wanajeshi hao wamekubali kuletwa nchini humo kwa wanajeshi 600 wa ECOWAS, akisema watachukua nafasi ya kikosi cha Angola ambacho kitaondoka nchini humo.

Wanajeshi hao walisema kuwa walifanya mapinduzi kuvunja mkataba kati ya serikali ya Gomes Junior na Angola, ambao wamedai ulikuwa ukilenga kuliangamiza jeshi la Guinea Bissau. Mapema mwezi huu, Angola ilitangaza kuachana na mkataba huo, baada ya mgongano na baadhi ya maafisa katika jeshi la Guinea Bissau.

Mwandishi wa shirika la habari la Reuters mjini Abidjan, amesema amemuona Carlos Gomes Junior akiwasili kwenye uwanja wa ndege mjini humo, akisafiri kwa ndege ya serikali ya Cote d'Ivoire, na kusindikizwa na mkuu wa jeshi la nchi hiyo, Jenerali Soumaila Bakayoko.

Ishara njema

Jumuiya ya ECOWAS imekuwa ikijitahidi kusuluhisha mizozo ya Afrika Magharibi

Jumuiya ya ECOWAS imekuwa ikijitahidi kusuluhisha mizozo ya Afrika Magharibi

Waziri wa Cote d'Ivoire ahusikaye na mshikamano wa kiafrika, Adama Bictogo, amesema kuachiwa kwa wanasiasa hao ni ishara kuwa wanajeshi wa Guinea Bissau wako tayari kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia. Alisema kuachiwa kwao ni ishara njema.

Bado haijulikani kikosi ni lini kikosi cha ECOWAS kitapelekwa nchini Guinea Bissau, lakini viongozi wamesema itabidi wapelekwe mara moja. Jeshi la kikanda litakuwa na jukumu la kumaliza uingiliaji wa kijeshi katika siasa za Guinea Bissau ambao ulianza mara tu baada ya uhuru, na kuchukua sura mpya baada ya kushamiri kwa biashara ya madawa ya kulevya kupitia kwenye kanda hiyo.

ECOWAS vile vile imesema inakusudia kupeleka kikosi kingine katika nchi ya Mali, ambako wanajeshi walifanya mapinduzi tarehe 22 Machi, na wanaendelea kuwa na ushawishi kisiasa licha ya kurudisha madaraka mikononi mwa serikali ya kiraia.

Mwandishi: Daniel Gakuba/RTRE

Mhariri: Stumai George

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com