Rais wa kipindi cha mpito ateuliwa Guinea Bissau | Matukio ya Afrika | DW | 20.04.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Rais wa kipindi cha mpito ateuliwa Guinea Bissau

Utawala wa kijeshi wa Guinea Bissau umemteua aliyekuwa mgombea wa urais, Manuel Serifo Nhamajo, kuwa rais wa serikali ya mpito. Jumuiya ya kimataifa imelaani hatua ya kuanzishwa kwa serikali.

Manuel Serifo Nhamadjo wa Guinea Bissau

Manuel Serifo Nhamadjo wa Guinea Bissau

Uteuzi wa Namhajo unakuja wiki moja baada ya wanajeshi kuipindua serikali ya Guinea Bissau. Nhamajo alikuwa miongoni mwa wagombea wa urais katika duru ya kwanza ya uchaguzi uliyofanyika mwezi uliyopita. Duru ya pili ilikuwa imepangwa kufanyika tarehe 29 mwezi huu, lakini mpango huo ulivurugwa na mapinduzi yaliyofanywa na wanajeshi. Uteuzi wa Nhamajo kuwa kiongozi wa serikali ya mpito ulifikiwa baada vyama 24 vya siasa vya Guinea Bissau kusaini makubaliano na utawala wa kijeshi.

Carlos Gomes Junior aliyetolewa madarakani

Carlos Gomes Junior aliyetolewa madarakani

Fernando Vaz, ambaye ni msemaji wa vyama vya upinzani, alitoa maelezo haya: "Kulingana na makubaliano ya kudumisha na kuboresha demokrasia, yaliyosainiwa na uongozi wa kijeshi na vyama mbalimbali vya siasa kwa lengo la kuunda serikali ya mpito ya kidemokrasia, tumemteua Serifo Nhamajo kuwa rais wa serikali ya mpito na Ibraima Sory Djaló kuwa rais wa baraza la taifa la mpito."

Katika tamko lake, chama cha PAIGC ambacho kilikuwa kumeunda serikali iliyopinduliwa, kimeeleza kwamba hakitatambua serikali ambayo haijahalalishwa na isiyokuwa ya kidemokrasia.

ECOWAS kuijadili Guinea Bissau

Wanajeshi wa Guinea Bissau

Wanajeshi wa Guinea Bissau

Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, jana ilisema kwamba hatua ya utawala wa kijeshi kuahirisha uchaguzi wa rais kwa muda wa miaka miwili inakwenda kinyume na sheria. Badala yake jumuiya hiyo inataka utawala wa kikatiba urudishwe mara moja na imeitisha mkutano wa dharura utakaofanyika wiki ijayo. "Kamisheni ya ECOWAS imeshangazwa na taarifa za kuundwa kwa kile kinachoitwa baraza la taifa la mpito linaloazimia kuiongoza Guinea Bissau kwa miaka miwili," ilieleza jumuiya hiyo katika tamko lililotolewa leo.

Baraza la Umoja wa Mataifa limeupinga uteuzi wa Serifo Nhamajo kuwa rais wa kipindi cha mpito. Akihutubia mbele ya baraza hilo, waziri wa mambo ya kigeni wa Ureno, Bw. Paulo Partas, ametoa wito wa kutokutolewa vibali vya kusafiria kwa viongozi wa serikali ya kijeshi na viongozi wa vyama pinzani vilivyo saini makubaliano ya kuunda serikali ya mpito.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/AFP/dpa

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman