1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Walioambukizwa corona duniani wapindukia milioni 18

Mohammed Khelef
3 Agosti 2020

Idadi ya walioambukizwa virusi vya corona duniani imepindukia milioni 18, ambapo milioni moja kati yao wamesajiliwa ndani ya kipindi cha masaa 24 yaliyopita, huku Marekani na Amerika Kusini zikiongoza.

https://p.dw.com/p/3gIfh
Großbritannien I Coronavirus I Manchester
Picha: Getty Images/AFP/O. Scarff

Marekani ndiyo iliyoathirika vibaya zaidi ikiwa na takribani watu milioni 4, 658,000, huku tayari taifa hilo kubwa kiuchumi na kijeshi duniani likiwa limeshapoteza watu 154,793 kwa maradhi ya COVID-19, likifuatiwa na Brazil yenye watu milioni 2, 734,000 walioambukizwa na vifo 94,104. 

Nchi ya tatu duniani kukumbwa zaidi na virusi vya corona ni India yenye wagonjwa milioni 1,750,723 na vifo 37,364. 

Mshauri wa masuala ya virusi vya korona wa Ikulu ya Marekani, Deborah Birx, ameonya kwamba sasa nchi hiyo imeshaingia kwenye "awamu mpya" ya janga hilo, kwani sasa maeneo ya vijijini yako hatarini kama yalivyo ya mijini. 

Akizungumza na kituo cha CNN, Birx ambaye anaongoza kikosi kazi cha corona kwenye Ikulu ya White House, amesema kwamba kinachoshuhudiwa sasa ni tafauti  na hali ilivyokuwa kwenye miezi ya Machi na Aprili, na kwamba watu wanaoishi mashamba hawako salama kama walivyo wa mijini.

Nchini Ujerumani, idadi ya watu waliothibitika kuambukizwa virusi vya corona imeongezeka kwa 509 na hivyo kufikia 210,402 hivi leo. Kwa mujibu wa Taasisi ya Robert Koch inayohusika na maradhi ya maambukizo, watu wengine saba wamepoteza maisha na kuifanya idadi ya waliokwishakufa kwa maradhi ya COVID-19 kufikia 9,148.

Asilimia 50 ya maambukizo ya Afrika yapo Afrika Kusini

Australien Melbourne | Coronavirus | Neue Corona-Einschränkungen
Polisi wakimlazimisha raia kuvaa barakowa nchini Australia.Picha: Imago Images/S. Low

Barani Afrika, nchi inayoongoza ni Afrika Kusini ambayo sasa ina wagonjwa 503, 290, ikiwa ni zaidi ya asilimia 50 ya maambukizo yote yaliyoripotiwa kwenye mataifa 54 ya bara hilo. Waziri wa Afya Zwelini Mkhize alisema watu 8,153 wameshapoteza maisha.

Taifa hilo lenye wakaazi milioni 58 ni la tano duniani kwa kuwa na watu wengi walioambukizwa virusi vya korona, likitanguliwa Marekani, Brazil, Urusi na India - yote yakiwa mataifa yenye idadi kubwa zaidi ya watu. 

Jimbo la Guateng, ambalo linajumuisha miji miwili muhimu ya Johannesburg na Pretoria, ndilo kituo kikuu cha maambukizo, ambapo asimilia 35 ya waliosajiliwa wanapatikana humo. Hospitali za jimbo hilo zinaelekea kuelemewa na wagonjwa, wakati wataalamu wakisema kilele hasa cha maambukizo kitakuwa mwishoni mwa mwezi huu wa Agosti au mwanzoni mwa Septemba.

Idadi ya waliosajiliwa kupoteza maisha kwa maradhi hayo duniani, imefikia sasa 687,941. Wataalamu wanasema idadi kamili ya watu walioambukizwa na wale waliokufa kwa korona inaweza kuwa kubwa zaidi ya hiyo ulimwenguni, kutokana na ukweli kwamba kiwango cha upimaji ni cha chini sana kulinganisha na uhalisia.