Waislamu washerehekea Eid Ul Fitr, baada ya Ramadhani
10 Aprili 2024Mamlaka nchini Saudi Arabia, taifa lenye misikiti miwili mitukufu kabisa kwa Waislamu, zilitangaza jioni ya jana kuwa waumini wa Kiislamu walitimiza siku 30 za kufunga na kwamba leo sala za iddi zitaswaliwa kote kwenye mamlaka hiyo.
Matangazo kama hayo yalisikika pia kutoka mamlaka za kidini za mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, Amerika, Arabuni, Ulaya na Asia.
Hapa nchini Ujerumani, Rais Frank-Walter Steinmeier ametuma salamu zake za Eid kwa Waislamu wa Ujerumani akiwapongeza kwa kukamilisha ibada ya mfungo wa Ramadhani, aliosema ni sehemu ya maisha ya jamii ya Kijerumani.
Ramadhani ni mojawapo ya nguzo tano za Uislamu, ambapo waumini wa dini hiyo hujizuwia kula, kunywa na mambo mengine yaliyokatazwa kwa mwezi mzima, kuanzia asubuhi hadi jioni kila siku.