Wagombea wa urais wa IAAF waahidi mageuzi | Michezo | DW | 14.08.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Wagombea wa urais wa IAAF waahidi mageuzi

Sergey Bubka na Sebastian Coe wanalenga kuzitunza taaluma zao kama maafisa wa michezo kwa kuchaguliwa kuwa rais wa Shirikisho la Kimataifa la Riadha – IAAF Jumatano wiki ijayo.

Wanariadha hao mashuhuri wa zamani wanapambana katika kinyang'anyiro cha urais wa IAAF wakiwa na ahadi za kufanya mageuzi yanayohitajika katika mchezo huo ikiwa watachaguliwa. Vigogo hao wawili wanawania kumrithi rais wa sasa Lamine Diack ambaye ameuongoza mchezo huo kwa miaka 16.

Coe mwenye umri wa miaka 58, alishinda dhahabu ya mbio za mita 1,500 katika Michezo ya Olimpiki ya 1980 na 1984 na akaishikilia rekodi ya ulimwengu katika mita 800 kwa miaka 16. Alikuwa kiongozi wa kamati ya maandalizi ya Michezo ya Olimpiki ya London 2012 na Makamu wa Rais wa IAAF na anapigiwa upatu kuchukua wadhifa wa rais.

Sergej Bubka Flash-Galerie

Sergey Bubka mgombea wa urais wa IAAF

Bubka, mwenye umri wa miaka 51, alileta enzi mpya katika mchezo wa kuruka kwa nguzo kwa kuruka mita 6 kwa mara ya kwanza na kuweka rekodi 35 za ulimwengu, ana mataji sita ya ulimwengu na dhahabu ya Olimpiki. Amekuwa Rais wa Kamati ya Olimpiki ya Ukraine, makamu wa rais wa IAAF na mwanachama wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki.

Wote wawili wanafahamu kuhusu jinamizi linaloliandamana mchezo wa riadha ambalo ni kukithiri matumizi ya dawa za kuongeza nguvu mwilini.

Bubka anasisitiza kuwa tabia hiyo haipaswi kukubalika kabisa kuendelea, na kuwa adhabu kali inapaswa kutolewa dhidi ya watumiaji wa dawa hizo, wakati Coe akitoa wito wa kuwepo mfumo huru kabisa wa kupambana na matumizi ya dawa hizo.

Kwa mujibu wa Coe, mashindano ya Diamond League yanahitaji hadhi sawa nay a mashindano makuu ya mchezo wa tennis maarufu kama Grand slam. Anasema ratiba ya mashindano ya riadha inapaswa kuwa na hadithi ya mwanzo, katikati na mwisho, na kuwa IAAF lazima itumie nguvu zake kuhakikisha kuwa mashindano makuu yana wanariadha bora zaidi ulimwenguni wanaojitokeza kushiriki. Kwa upande wake, Bubka anapendekeza kuwa mashindano ya Diamond League yapewe jina jipya la Kombe la Dunia la IAAF.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Daniel Gakuba