1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafuasi wa Katumbi waridhishwa kuruhusiwa kuwania urais DRC

Jean Noël Ba-Mweze
31 Oktoba 2023

Wafuasi wa kiongozi wa upinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Moise Katumbi, wamefurahishwa na uamuzi wa Mahakama ya Katiba uliomfungulia njia ya kugombea uchaguzi wa rais wa Disemba 20.

https://p.dw.com/p/4YET7
Mgombea urais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya kutoka upinzani, Moise Katumbi.
Mgombea urais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya kutoka upinzani, Moise Katumbi.Picha: Nicolas Maeterlinck/BELGA/dpa/picture alliance

Mapema, Katumbi na rais wa sasa, Felix Tshisekedi, walikuwa wamefikishwa mahakamani kuhusu masuala ya migogoro ya uchaguzi.

Lakini mbali ya kuwaruhusu wawili hao, Mahakama hiyo ya Katiba iliwakubalia pia wagombea wengine wawili kuwania urais, ambao hapo kabla Tume Huru ya Uchaguzi (CENI), ilikuwa imekataa maombi yao.

Soma zaidi: Katumbi aibua muungano vyama tawala Kongo

Mahakama Kuu DRC yatupilia mbali kesi ya kumzuia Katumbi kuwania urais

Ingawa wafuasi wa Katumbi walikuwa awali wakikasirika na hata kupinga uamuzi kabla ya kutolewa, sasa wanasema wameridhishwa.

"Sisi tunataka kuwe na sheria iliyo huru kwani hata rais mwenyewe anakuwa akilaumu kila mara jinsi sheria inavyoendeshwa hapa. Tukishinda uchaguzi huu tutaifanya Kongo kuwa nchi ya sheria. Sharti sheria iwe juu ya wote. Tunayofanya leo ni madogo na bado tupo mwanzoni mwa mapambano marefu." Alisema mmoja wa wafuasi wa Katumbi, Francis Kalombo, kwenye mazungumzo yake na mwandishi wa DW mjini Kinshasa.

Tuhuma dhidi ya Katumbi

Katumbi alishitakiwa na mgombea mwenzake wa urais, Noël Tshiani, kwa ukosefu wa uraia wa asili ya Kongo, lakini kwenye hukumu yake, Mahakama ya Katiba ilisema siku ya Jumatatu (Oktoba 30) kwamba "shitaka hilo halina msingi."

Wafuasi wa Moise Katumbi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Wafuasi wa Moise Katumbi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.Picha: JOHN WESSELS/AFP

Kwa upande wake, Rais Tshisekedi alishitakiwa na mgombea Seth Kikuni kwa kubadili jina lake.

Licha ya Mahakama kukubali kupokea mashitaka hayo, ilisema pia kwamba hayana msingi wowote wa kisheria.

Soma zaidi: Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kufanya uchaguzi mkuu Desemba 2023.

Kwenye kesi nyengine ya migogoro ya uchaguzi, Mahakama hiyo ya Kikatiba ilikubali pia wagombea wengine wawili, Enock Ngila na Joëlle Bille, ambao fomu zao zilikuwa zimekataliwa na CENI kuwania uchaguzi huo.

Kwa uamuzi huo wa Mahakama ya Katiba, sasa ni rasmi kuwa uchaguzi wa rais wa tarehe 20 Disemba 2023 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo utakuwa na wagombea 26, wawili kati yao wakiwa wanawake.

CENI yasema uchaguzi upo kama ulivyopangwa

Mwenyekiti wa CENI, Denis Kadima, aliuambia ujumbe wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika ya Kati ulioongozwa na kamishna wa wa masuala ya kisiasa, amani na usalama wa jumuiya hiyo, Mangaral Bante, kwamba uchaguzi utakuwepo kama ulivyopangwa.

Baadhi ya wagombea wa urais wa Kongo kwa uchaguzi wa Disemba 20. Kutoka juu kushoto: rais wa sasa Felix Tshisekedi, Moise Katumbi, Dennis Mukwege na Martin Fayulu.
Baadhi ya wagombea wa urais wa Kongo kwa uchaguzi wa Disemba 20. Kutoka juu kushoto: rais wa sasa Felix Tshisekedi, Moise Katumbi, Dennis Mukwege na Martin Fayulu.Picha: AFP/Getty Images, picture alliance, G. Kusema, DW

Bante aliwaambia waandishi wa habari kwamba Kadima aliwaeleza kuhusu matatizo ambayo CENI inakumbana nayo ila aliwaonesha pia jinsi mambo yanavyoendelea.

Soma zaidi: Wagombea wanawake ni wachache uchaguzi wa DRC - CAFCO

"Maandalizi yanaendelea vyema na alisisitiza kuwa muda na tarehe za mchakato zitaheshimiwa kuhusu uchaguzi kufanyika." Alisema Bante.

Wakongo wanatarajiwa kumchagua rais, wabunge wa kitaifa na wa mikoa, pamoja na washauri wa manispaa kwenye uchaguzi wa mwaka huu.

Imetayarishwa na Jean Noël Ba-Mweze/DW Kinshasa