Wademokrat wapata mwenyekiti mpya | Matukio ya Kisiasa | DW | 26.02.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Wademokrat wapata mwenyekiti mpya

Wanachama wa chama cha Demokrat nchini Marekani Jumamosi (25.02.2017) wamemchaguwa Tom Perez veterani wakati wa utawala wa rais Barack Obama kuongoza mapambano dhidi ya Rais Donald Trump na wabunge wa Repulikan bungeni.

US-Demokraten wählen neunen Parteivorsitzenden Tom Perez (picture alliance/AP Photo/B. Camp)

Mwenyekiti mpya wa chama cha Demokrat Tom Perez

Tom Perez aliyekuwa waziri wa kazi chini ya utawala wa rais wa zamani Barack Obama na kiongozi mlatino wa kwanza amemtangaza mara moja mtu aliyeshika nafasi ya pili mbunge wa sera za mrengo wa kushoto Keith Ellison kuwa naibu mwenyekiti wa chama hicho.

"Kuna siku wataisoma enzi hii katika historia ya Marekani kuuliza suali kwetu sote mlikuwa wapi mwaka 2017 wakati tulipokuwa na rais mbaya kabisa  kuwahi kushuhudiwa katika historia ya Marekani?." amesema Perez mwenye umri wa miaka 55.

"Na tutaweza kuwajibu chama kilichoungana cha Demokrat kiliongoza upinzani kuhakikisha rais huyo anakuwa wa kipindi kimoja na kuwachaguwa Wademokrat nchini kote.

Ellison aweka historia


US-Demokraten wählen neunen Parteivorsitzenden Keith Ellison (picture alliance/AP Photo/B. Camp)

Naibu mwenyekiti wa chama cha Demokrat Keith Ellison

Ellison Mmarekani-Mweusi mwenye umri wa miaka 53 ambaye ni Muislamu wa kwanza kuchaguliwa katika bunge la Marekani ameonya kwamba "hatuna ufahari kutoka katika chumba hiki ikiwa tumegawika".

Mapambano juu ya nani anapaswa kuwa mwenyekiti wa kamati ya taifa ya chama cha Demokrat wakati fulani yalionekana kama mapambano baina ya mawakala baina ya wafuasi wa mgombea urais aliyeshindwa katika uchaguzi wa rais 2016 Hillary Cilinton na mpinzani wake wakati wa chaguzi za mchujo Bernie Sanders.

Perez alipata kura 235 dhidi ya kura 200 alizopata Ellison mfuasi mkubwa wa Sanders ambaye alionekana kuwa chaguo la serikali ya wakati wa Obama.

Peter Buttiging mgombea shoga aliyepata nafasi

Mgombea watatu Meya wa South Bend Indiana Peter Buttiging ambaye ni shoga mwenye umri wa miaka 35 na Rhodes Scholar veterani wa kijeshi walijitowa katika kinyan'ganyiro hicho kabla ya kura kuanza kupigwa katika uchaguzi huo uliofanyika katika mji wa Atlanta katika jimbo la Georgia.

Tafauti na chaguzi zinazofanyika katika nchi za kidemokrasia vyama hivyo viliwili vikuu vya kisiasa nchini Marekani vina ushawishi mdogo katika suala la sera wakati wabunge wakuu wa chama wakiwa na usemi zaidi.

Lakini dhima yao hiyo ya nyuma ya pazia inazidi kuwa na umuhimu kufuatuia kushundwa kwa Clinton katika uchaguzi wa mwaka 2016  na wakati wanachama hao wa Demokrat wakijiandaa kwa ajili ya chaguzi za kipindi cha kati mwakani na uchaguzi wa rais mwaka 2020.

Perez ambaye anachukuwa nafasi ya mwenyekiti wa muda Donna Brazile ameshika nafasi hiyo baada ya kuondolewa kwa Mwakilishi Debbie Wasserman Schulz katikati ya mwaka 2016 wakati baruwa pepe zilizovuja kuonyesha kwamba baadhi ya wajumbe wa kamati ya taifa ya chama hicho ambao waliahidi kutokuwa na upendeleo katika chaguzi za mchujo za urais walimpendelea Clinton dhidi ya Sanders.

Kumchaguwa Perez " ni kupoteza fursa nyengine kwa chama cha Demokrat ambacho kinajaribu kurudisha tena umuhimu wake na kuthibitisha jinsi watu wa ndani wa chama walivyokuwa mbali na mavuguvugu ya ngazi ya chini ambayo hivi sasa yako mitaani " hayo yamesemwa na Jim Dean wenyekiti wa kundi la wafuasi wa Ellison.

Lakini Obama ambaye kwa kiasi kikubwa amekuwa kimya tokea aondoke madarakani hapo mwezi wa Januari ametowa wito wa kusuluhisha tofauti zao.   

Perez amesema "wakati tunapoongoza na ujumbe wetu, ujumbe wetu wa fursa za kiuchumi hivyo ndivyo tunavyoshinda"

Perez pia ameonya kwamba Wademokrat lazima waufanyie mageuzi mfumo wao wa chaguzi za mchujo kupata mgombea urais ambao amesema umesababisha "mzozo wa imani "kwa sababu ya kukosa uwazi.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP

Mhariri: Sudi Mnette           

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com