1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wabunge wa Congo wasusia vikao vya bunge

Amina Mjahid
20 Aprili 2022

Wabunge kutoka mikoa ya Kivu Kaskazini na Ituri Mashariki mwa DRC wamegoma kuhudhuria vikao vya bunge mjini Kinshasa wakitaka kuondolewa kwa uongozi wa kijeshi uliowekwa na Rais Felix Tshisekedi

https://p.dw.com/p/4A8g8
DRK Symbolbild Polizei
Picha: Alexis Huguet/Getty Images/AFP

Wabunge hao wanasema badala ya kuimarika kwa usalama, kumekuwa na ongezeko la mauaji dhidi ya raia yanayofanywa na makundi ya waasi  katika mikoa hiyo miwili.

Haya yanajiri siku chache tu baada wabunge hao kutoka mikoa ya Kivu Kaskazini na ituri kuwasilisha ripoti iliyochapishwa mapema mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye Ofisi ya Rais Tshisekedi, inayoonesha kuwa zaidi ya watu elfu 5 waliuawa kwa risasi pamoja na nyumba zaidi ya 380 kuchomwa moto tangu kutangazwa kwa ungozi huu wa kijeshi na kuongeza hofu katika baadhi ya vjiji kwenye mikoa yote hiyo miwili.

Badala ya utawala wa kijeshi uliowekwa na Rais Tshisekedi, wabunge hao wamependekeza kuimarishwa kwa vikosi vya jeshi la Congo, FARDC, pamoja na huduma nyingine za usalama kama kuwatolewa vifaa maalumu vya vita ili kuendelea kukabiliana na kundi la ADF-Nalu pamoja  na makundi mengine ya waasi katika maeneo yote yanayokumbwa na machafuko.

Mashirika ya kiraia yaunga mkono hoja ya wabunge

Felix Tshisekedi | Präsident Demokratische Republik Konogo
Rais wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi Picha: Arsene Mpiana/AFP/Getty Images

Upande wa mashirika ya kiraia ambayo yamekuwa yakilikosoa jeshi la Kongo tangu kuanzishwa kwa operesheni za kijeshi dhidi ya makundi ya wapiganaji katika miko ya Kivu Kaskazini na Ituri yameunga pia mkono wabunge hao na kuwataka kuondoka Kinshasa, wakidai ndio njia pekee inayoweza kuwasaidia maelfu ya raia kupata matumaini ya amani.

Haya yanajiri wakati kwenye jijini Kinshasa, wabunge zaidi ya 100 wa vyama vya upinzani wametangaza kugomea vikao vya bunge vinavyojadili sheria na kanuni mpya za uchaguzi, wakilalamikia kile wanachokiita uingiliaji kati wa Rais Tshisekedi kwenye mfumo wa uchaguzi kwa ajili ya kujipendelea.

Hapa mashariki mwa Kongo, Bunge hilo la Jamhuri limeshaongeza muda wa hali ya dharura katika mikoa ya Kivu Kaskazini na Ituri kwa mara ya 22 wakati bado waasi wa kundi la ADF-Nalu pamoja na makundi mengine kadhaa ikiwemo lile la CODECO yanaendelea kuvuruga usalama wa raia na kuwatumbukiza maelfu katika hali ya umaskini.

Mwandishi: Benjamin Kasembe/DW Goma