Waasi wauteka mji wa kaskazini Mali | Matukio ya Afrika | DW | 22.04.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Waasi wauteka mji wa kaskazini Mali

Waasi wameuchukua mji wa kaskazini mwa Mali baada ya mapigano kati yao na wanamgambo wa kundi linalodai uhuru wa jimbo la Azawad ikiwa ni miezi mitatu tu tangu Ufaransa kuwang'oa wanamgambo wa Kiislamu kutoka eneo hilo.

Shirika la habari la AP limemnukuu afisa mmoja wa serikali ya Mali akisema kwamba mapigano yalizuka karibu ni mji wa Timbuktu kati ya waasi wa Tuareg wanaopigania kuwa na serikali isiyofuata dini na wanamgambo wa Harakati za Waarabu wa Azawad (MAA) usiku wa kuamkia leo (tarehe 22.04.2013).

Mukhtar Oud Suleiman, afisa wa serikali kwenye mji wa Ber, amesema kwamba magari matano ya waasi wa Kiarabu yaliwasili kwenye mji huo, wakisema kwamba walikuja kuwafukuza waasi wa Tuareg ambao wamekuwa wakishutumiwa kwa kushambulia biashara zinazomilikiwa na Waarabu.

Kwa mujibu wa msemaji wa wanamgambo hao wa Kiarabu, Mohammed el-Mauloud Ramadhan, wao ndio sasa wanaoshikilia mji huo ulio umbali wa kilomita 50 mashariki ya Timbuktu. Ramadhan ameliambia shirika la habari la AFP kwamba lengo lao ni kuulinda mji huo dhidi ya makundi yenye silaha "yanayowakera wazazi" wao.

"Tunataka kushirikiana na wanajeshi wa Ufaransa na wa Kiafrika wanaopambana dhidi ya ugaidi na usafirishaji wa madawa ya kulevya." Amesema Ramadhan.

Bado hali ni mbaya

Wakimbizi wa Kituareg nchini Burkina Faso.

Wakimbizi wa Kituareg nchini Burkina Faso.

Taarifa za waasi wa MAA kuudhibiti mji wa Ber zimethibitishwa pia na chanzo kimoja kwenye jeshi la Mali. Wachunguzi wa mambo wanasema hili linaashiria ukweli kwamba bado hali ingali tete kaskazini mwa Mali, miezi mitatu baada ya wanajeshi wa Ufaransa kutangaza kuwang'oa wanamgambo wanaofuata siasa kali za kidini kutoka eneo hilo.

Ufaransa iliingilia kati kijeshi kwenye koloni hilo lake la zamani mwezi Januari, ikisema inakusudia kuwazuia waasi wa Ansaruddin wenye mafungamano na al-Qaida kuuchukua mji mkuu wa Mali, Bamako. Waasi hao walishafanikiwa kuidhibiti miji kadhaa ya kaskazini tangu mwezi Aprili 2012.

Lakini hata baada ya Ufaransa kulirudisha tena eneo la kaskazini kwenye udhibiti wa serikali na kuwalazimisha wanamgambo hao wa Kiislamu kukimbilia mafichoni kwenye majangwa, kumeibuka vita vipya vya kuvizia vinavyojumuisha mashambulizi ya kushitukiza, mabomu ya kujitoa muhanga na ya kutegwa ardhini.

Vyanzo kadhaa vya habari vimeliambia shirika la habari la AFP kwamba, wapiganaji wapatao 200 wa kundi lililojitenga na Ansaruddin la Harakati za Kiislamu la Azawad, MIA, linaelekea kwenye mji wa Kidal, kwa kile kiongozi wa kundi hilo, Alghabass ag Intallah, alichokiita "kuipima serikali mjini Bamako ikiwa inataka amani ama la!"

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/AFP
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman

DW inapendekeza